Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Iran (SNSC), Mohammad Baqer Zolqadr, ametoa jibu madhubuti kwa vitisho vya hivi karibuni vya Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya taifa la Iran, akisisitiza kwamba Tehran haitavumilia lugha isiyo na heshima na itajibu ipasavyo ikiwa italazimu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval, Trump alidai jana Jumatatu kwamba Marekani itashinda vita vya Iran “kwa njia moja au nyingine.”

“Tutafanya makubaliano, au tutamaliza kazi. Haitakuwa vigumu kumaliza kazi,” Trump alitangaza.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu, Zolqadr alimhutubu moja kwa moja Rais wa Marekani, akisema kuwa “amepatwa na umajnuni” kwa kuwatishia watu milioni 91 wa Iran.

“Kwa Rais wa Marekani mwenye njozi, ambaye leo amewatishia Wairani milioni 91, nasema: Hapo awali, kama rais wa nchi isiyo na mizizi yenye historia ya miaka 250 tu, ulizungumza kwa maneno kama hayo kuhusu kufuta ustaarabu wa Iran wenye umri wa miaka elfu kadhaa. Matokeo pekee kwako yalikuwa kushindwa, kupatwa na ajizi na kuomba kufanya mazungumzo na kusitisha mapigano,” amesema Zolqadr.

Amesisitiza kwamba Wairani hawajui na hawaguswi na lugha ya vitisho vya ajinabi.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Iran amemwambia Trump kwamba: “Wairani hawajui lugha ya vitisho. Kwa hivyo, zungumza na watu wa Iran kwa heshima; la sivyo, tutakujibu kwa lugha tofauti.”

Matamshi hayo yametolewa kupinga waziwazi vitisho vya mara kwa mara vya Washington dhidi ya Iran.

Maafisa wa Iran wamesisitiza mara kwa mara kwamba Jamhuri ya Kiislamu na watu wake wenye fahari hawatakubali kamwe uonevu au maneno yasiyo na heshima kutoka kwa Marekani.

Tehran imeweka wazi mara kwa mara kwamba uchokozi wowote au kiburi kitakabiliwa na jibu imara, lililopangwa na linalofaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *