Dar es Salaam. Viongozi kutoka Tanzania, Zambia na China wamewataka wadau kuhakikisha Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) inafufuliwa na kuimarishwa ili kuendeleza urithi ulioachwa na wafanyakazi waliopoteza maisha wakati wa ujenzi wake zaidi ya miaka 50 iliyopita.

Wito huo umetolewa leo Julai 7, 2026 katika ibada maalumu ya kuwaenzi wafanyakazi hao iliyofanyika katika Makaburi ya Wataalamu wa China yaliyopo Gongo la Mboto, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya Tazara.

Akizungumza katika ibada hiyo, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema reli hiyo ni alama ya urafiki, mshikamano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya China, Tanzania na Zambia, uliojengwa kwa kujitolea kwa maelfu ya wafanyakazi.

Amesema zaidi ya wataalamu na wafanyakazi 50,000 kutoka China walishiriki ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860 inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kapiri Mposhi nchini Zambia, huku wafanyakazi 70 wa China wakipoteza maisha wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

“Kumbukumbu hii inatukumbusha kujitolea kwa mashujaa hao na kutupa wajibu wa kuendeleza ‘Roho ya TAZARA’ inayojengwa katika misingi ya urafiki, usawa, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa,” amesema.

Chen amesema ushirikiano kati ya China na Tanzania umeendelea kuimarika kwa miaka mingi, huku China ikiendelea kuwa mshirika mkubwa wa biashara wa Tanzania kwa zaidi ya muongo mmoja.

Ameongeza kuwa mradi wa kuifufua Tazara uliozinduliwa Novemba mwaka jana unalenga kuiboresha reli hiyo ili kuongeza biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Bruno Ching’andu, amesema reli hiyo si miundombinu pekee, bali ni urithi uliojengwa kwa maono, dhamira na kujitoa kwa maelfu ya watu waliokuwa tayari kutoa maisha yao.

Amesema ujenzi wa reli hiyo ulikuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kihandisi kuwahi kutekelezwa barani Afrika, ambapo wafanyakazi kutoka Tanzania, Zambia na China walifanya kazi katika mazingira magumu ili kuunganisha mataifa hayo.

“Heshima kubwa tunayoweza kuwapa waliopoteza maisha si kufanya ibada za kumbukumbu pekee, bali kuhakikisha reli waliyoijenga inaendelea kuhudumia wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi kwa vizazi vijavyo,” amesema.

Kwa mujibu wa Ching’andu, juhudi za kuifufua Tazara zinalenga kuirejesha katika ubora wake, kuongeza ufanisi na ushindani, huku ikidumisha maono ya waasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda.

Naye Kamishna Mkuu wa Zambia nchini Tanzania, Mathews Athews Jere, amesema Tazara ilitoa mchango mkubwa kwa Zambia kwa kuiwezesha kupata njia ya uhakika ya kufikia bahari katika kipindi cha changamoto za kisiasa na kiuchumi.

Amesema reli hiyo ni ushahidi wa maono ya viongozi waasisi wa Tanzania na Zambia kwamba ushirikiano wa Afrika unaweza kutatua changamoto kubwa za maendeleo.

“Wengi waliziacha familia zao kwa miaka kadhaa na baadhi yao hawakurejea tena. Leo tunawakumbuka mashujaa hao ambao sadaka yao imeendelea kuwanufaisha mamilioni ya wananchi kwa zaidi ya miaka 50,” amesema.

Ameishukuru Serikali za Tanzania na China kwa kuendelea kushirikiana katika kuendeleza reli hiyo, akisisitiza kuwa njia bora ya kuwaenzi waliopoteza maisha ni kuhakikisha Tazara inaendelea kuwa mhimili wa biashara, usafirishaji na maendeleo kwa vizazi vijavyo.

Maadhimisho ya miaka 50 ya Tazara yanaendelea nchini Tanzania na Zambia kupitia shughuli mbalimbali zinazolenga kuenzi historia ya reli hiyo na kuimarisha dhamira ya kuifanya iendelee kuwa nguzo muhimu ya uchumi na ushirikiano wa kikanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *