Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) limetumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya usafiri majini, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama wa vyombo vya majini na fursa zinazopatikana katika uchumi wa buluu.

Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum, amesema mwitikio mkubwa wa wananchi na wadau wanaotembelea banda la shirika hilo unaonyesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Tasac pamoja na nafasi za uwekezaji zilizopo katika sekta hiyo.

Akizungumza Julai 6, 2026 baada ya kutembelea banda la Tasac, Salum amewashukuru wananchi na wadau waliofika kujionea shughuli za shirika hilo, huku akiwahamasisha wengine kutumia maonesho hayo kupata uelewa wa kina kuhusu usalama wa usafiri majini na fursa za biashara.

“Nawashukuru wadau na wananchi wote waliotembelea banda la Tasac. Ninawahimiza wengine wajitokeze ili wajifunze zaidi kuhusu huduma zetu pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara zilizopo katika sekta ya usafiri majini,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed  Salum akizungumza baada ya kutembelea banda la shirika hilo Sabasaba.

Amesema maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa Tasac kufikisha elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya kusimamia usalama, ulinzi na ubora wa huduma za usafiri majini, huku yakichochea uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo.

Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yalianza Juni 28 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026, yakishirikisha taasisi za umma na binafsi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Katika hatua nyingine, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, ametembelea banda la Tasac na kupata maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo, zikiwemo usajili na ukaguzi wa vyombo vya majini, usimamizi wa sheria na kanuni za usafiri majini pamoja na juhudi za kulinda mazingira dhidi ya uchafuzi unaotokana na shughuli za meli.

Baada ya ziara hiyo, Rugwa amelipongeza Tasac kwa mchango wake katika kuimarisha usalama wa usafiri majini, akisema hatua zilizochukuliwa na shirika hilo zimechangia kupunguza ajali majini na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi salama ya vyombo vya usafiri wa majini.

Amesema mafanikio hayo yanaunga mkono juhudi za Serikali za kulinda maisha ya wananchi na kuhifadhi mazingira ya bahari na maji ya ndani kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, ameshauri Tasac kuendelea kutumia maonesho ya umma kama Sabasaba kuelimisha wananchi na wadau kuhusu majukumu yake ili kuongeza uzingatiaji wa viwango vya usalama katika sekta ya usafiri majini.

Pia amezitaka kampuni zinazojihusisha na usafirishaji wa mizigo kutumia bandari kavu zilizopo Morogoro, Pwani na Dodoma ili kusaidia kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *