
TIMU ya Wembe iliyopanda daraja kushiriki Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2026-2027, ipo katika mazungumzo na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Fufuni, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’ kwa lengo la kuinoa timu hiyo.
Taarifa kutoka Wembe yenye maskani yake Pemba, zinaeleza klabu hiyo imevutiwa na uwezo wa Gamera ambaye msimu wa 2025-2026 aliiongoza Fufuni ikiwa imepanda daraja na kuzisumbua timu vigogo kabla ya kuwekwa pembeni hali iliyofanya timu hiyo kuyumba dakika za mwisho.
“Gamera anatakiwa na Wembe kwani viongozi wanaamini ni kocha ambaye ana uwezo mkubwa wa kufundisha timu na kufanya vizuri kwenye ligi. Mazungumzo bado yanaendelea, yakiwa mazuri basi atatangazwa,” kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Mwanaspoti lilimtafuta Gamera na alisema hadi sasa hajafanya uamuzi wowote wa kukubali kufanyakazi na timu hiyo kwani anahofia kujirudia kilichomtokea kwa Fufuni ambayo nayo inatokea Pemba.
“Kweli timu ya Wembe imenitafuta ili niwe kocha mkuu wao, lakini nahofia kurejea ya Fufuni, kwa maana hiyo bado sijafanya uamuzi,” alisema kocha huyo.
Gamera alisema amepatwa na uoga kufundisha timu zinazotokea kisiwani Pemba huku akidai timu za huko hazina shukurani zaidi ya matusi.
Alieleza amefundisha timu nyingi kisiwani Unguja ila kwa upande wa Pemba msimu wa 2025-2026 ilikuwa mara yake ya kwanza na alikaribishwa vibaya.
Gamera alisema mbali na hilo bado hajapata jibu la moja kwa moja aende Wembe au la, matamanio yake makubwa msimu ujao kupata timu kutokea Tanzania Bara kwa sababu uwezo wa kuzinoa timu za huko anao.