WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Tanzania inapaswa kuwekeza zaidi katika tafiti za kisayansi na kuimarisha uwezo wa ndani wa kugundua, kutengeneza na kuzalisha dawa zitakazotatua changamoto za afya zinazowakabili Watanzania.
Profesa Mkenda alitoa kauli hiyo Julai 8, 2026, alipotembelea Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) katika kituo chake cha Bagamoyo, ambako alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za utafiti, maabara za kisasa, majaribio ya kitabibu na bunifu zinazotekelezwa na watafiti wa taasisi hiyo.
Amesema Tanzania ina rasilimali watu, wataalamu na malighafi za kutosha, hivyo kinachohitajika ni kuwekeza katika tafiti, vifaa vya kisasa na mazingira yatakayowezesha wanasayansi kufanya kazi kwa ufanisi.”Hatufanyi hivyo kwa ajili ya kutafuta fedha; tunafanya hivyo kwa ajili ya kuboresha afya za Watanzania, lakini baadaye tutapata pia mshiko.”
Profesa Mkenda amesema dawa zinazotokana na tafiti za ndani zinapaswa kupitia hatua zote muhimu za kisayansi, ikiwemo majaribio ya awali (pre-clinical trials) nchini kabla ya kuendelea na majaribio kwa binadamu, ili kujiridhisha kuhusu usalama na ufanisi wake.
Pia amesema baada ya kuthibitishwa kuwa dawa hizo ni salama, Serikali na taasisi husika zinapaswa kuhakikisha nchi inanufaika na haki miliki ya teknolojia ya uzalishaji wa dawa hizo badala ya kutegemea mataifa mengine.
Aidha, ameitaka Wizara ya Elimu Sayansi, na Teknolojia kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, taasisi zinazoshughulikia tiba asili, vyuo vikuu na taasisi za utafiti kukutana na kuweka mkakati wa pamoja wa kufanya tafiti kuhusu miti tiba ili kubaini uwezo wake wa kutibu magonjwa mbalimbali na kuwezesha utengenezaji wa dawa zinazokidhi viwango vya kisayansi.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na wanasayansi wengi wenye uwezo mkubwa wa kufanya tafiti na kugundua tiba mbalimbali, lakini wanahitaji kupewa mazingira bora, fedha na miundombinu ya kisasa ili maarifa yao yaweze kuleta matokeo yanayoonekana.
Profesa Mkenda amesema kuna haja ya kuboresha maabara za utafiti kwa kuzinunulia mashine za kisasa zitakazowezesha uchunguzi wa kina wa sampuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mashine za teknolojia ya vinasaba ambazo bado ni chache nchini.

Ametolea mfano tafiti za chanjo ya malaria na kusema Serikali inapaswa kuwa na mpango wa muda mrefu wa kununua vifaa vya kisasa vya utafiti badala ya kusubiri misaada, jambo litakaloongeza uwezo wa nchi kufanya tafiti zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Pia amesema ziara ya Rais nchini Urusi imefungua fursa mpya za ushirikiano katika elimu ya juu, sayansi na teknolojia, hivyo Tanzania inapaswa kuzitumia kuwapeleka wanafunzi na watafiti katika vyuo na taasisi za utafiti ili kupata utaalamu katika maeneo mapya kama bioteknolojia, vinasaba na utengenezaji wa dawa.
“Hatuna sababu ya kuwasomesha wanasayansi kama bado hatuwezi kuwatumia. Tukishindwa kuwapa mazingira ya kufanya tafiti na kutumia taaluma zao, tutakuwa hatujafanya jambo la msingi kwa maendeleo ya Taifa.”
Katika ziara hiyo, ujumbe wa Waziri ulipata maelezo kuhusu historia ya Taasisi ya Afya Ifakara ambayo mwaka huu inaadhimisha miaka 70 ya kufanya tafiti za afya nchini pamoja na mchango wake katika mapambano dhidi ya malaria, kifua kikuu, magonjwa ya kuambukiza na afya ya mama na mtoto.
Ujumbe huo pia ulitembelea Kitengo cha Majaribio ya Kitabibu, maabara za utafiti, mradi wa Transmission Zero unaolenga kutokomeza maambukizi ya malaria na vituo vya mafunzo vinavyowaandaa watafiti wa ndani na kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Profesa Mkenda amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti, vyuo vikuu na sekta binafsi ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanageuzwa kuwa sera, teknolojia, dawa na bidhaa nyingine zitakazoboresha huduma za afya, kukuza uchumi na kuongeza uwezo wa Tanzania kujitegemea katika sekta ya sayansi na teknolojia.