Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amemtaka Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Massana Mwishawa, kuhakikisha anajenga nidhamu isiyotetereka kwa maofisa na askari wa uhifadhi kwa kusimamia uzingatiaji wa sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao na kusimamia maslahi yao.

Amesema Serikali haitavumilia vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, utovu wa nidhamu, matumizi mabaya ya mali za Serikali wala vitendo vinavyochafua taswira ya Tanapa na Serikali kwa ujumla.

Waziri huyo amesema hayo leo Alhamisi, Julai 9, 2026, katika hafla ya kumvisha cheo na kumuapisha Mwishawa katika Makao Makuu ya Tanapa yaliyopo mkoani Arusha.

Amesema moja ya matarajio makubwa ya Serikali ni kuendelea kuhamasisha nidhamu, uwajibikaji na ustawi wa watumishi wa Tanapa.

“Jeshi la Uhifadhi ni uti wa mgongo wa uhifadhi wa hifadhi za taifa letu. Ufanisi wa Tanapa katika kulinda bioanuwai, kupambana na ujangili, kudhibiti uvamizi na kulinda rasilimali za taifa unategemea kwa kiwango kikubwa uwepo wa maafisa na askari wenye nidhamu, uadilifu, uzalendo na weledi wa hali ya juu.

“Kwa hiyo ninakuelekeza kuhakikisha unajenga nidhamu isiyotetereka kwa maafisa na askari wetu. Wahakikishe wanazingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao,” amesema Dk Kijaji.

“Serikali haitavumilia vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, utovu wa nidhamu, matumizi mabaya ya mali za Serikali wala vitendo vyovyote vinavyochafua taswira ya Tanapa na Serikali kwa ujumla,” amesema

Waziri huyo amesema Serikali ina matarajio makubwa kwa Mwishawa kutokana na uzoefu wake ndani ya Tanapa, akimtaka kuimarisha ustawi wa watumishi kwa kuhakikisha maslahi na stahiki zao zinapewa kipaumbele na kulipwa kwa wakati.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha nyumba za watumishi na askari, kuongeza vitendea kazi, kuimarisha mafunzo pamoja na kuboresha huduma za afya kwa kuwa mtumishi mwenye motisha ndiye msingi wa taasisi yenye mafanikio.

Aidha, amemwelekeza Mwishawa kuongeza ushirikiano na sekta binafsi ili kuongeza idadi ya vitanda vya malazi ndani ya hifadhi, sambamba na kuweka wazi maeneo yote ya uwekezaji yaliyopo ili kuvutia wawekezaji, wakati Tanzania ikijiandaa kupokea wageni wa Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) utakaofanyika Arusha Oktoba mwaka huu na Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Akizungumza baada ya kuapishwa, Kamishna Mwishawa amesema katika kutekeleza wajibu wake atazingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji wa pamoja, nidhamu, uzalendo na ubunifu ili kupata matokeo yenye tija.

“Dhamira yangu ni kuendelea kuijenga Tanapa inayotekeleza majukumu yake kwa weledi wa hali ya juu na hatimaye kutoa huduma bora kwa wateja wake wote, katika uongozi wangu nitajikita zaidi katika kuhakikisha mazingira ya kazi kwa watumishi pamoja na maslahi yao yanaendelea kuboreshwa, ukusanyaji wa mapato ya Serikali unaongezeka,”amesema na kuongeza

“Ulinzi wa maliasili unaendelea kuimarishwa, shughuli za utalii zinaendelea kuboreshwa, miundombinu ya utalii ikiwemo barabara na viwanja vya ndege inaendelea kuboreshwa, pamoja na kuboresha mahusiano na jamii zinazozunguka hifadhi za taifa.”

“Hifadhi za Taifa ni hazina ya kiikolojia, kiuchumi, kijamii, kisayansi na kitamaduni. Hifadhi hizi zina mchango mkubwa kwa taifa, ikiwemo kuchangia kuzalisha mapato ya Serikali, kutoa mchango wa maendeleo kwa jamii zinazozunguka hifadhi na kuwa chanzo muhimu cha maji yanayotumika katika miradi mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo uzalishaji wa umeme hapa nchini,” amesema

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tanapa, Jenerali Mstaafu George Waitara, amesema Bodi ina imani na uwezo wa Mwishawa kutokana na kupitia ngazi mbalimbali za utumishi ndani ya shirika hadi kufikia nafasi ya Naibu Kamishna wa Uhifadhi.

Alimtaka Mwishawa kuimarisha uwajibikaji wa pamoja na kujenga utamaduni wa kufanya kazi kama timu, akieleza kuwa ushirikiano ndiyo msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote. Amesema Bodi ya Wadhamini iko tayari kutoa ushauri na ushirikiano wakati wowote utakapohitajika ili kuhakikisha Tanapa inafikia malengo yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *