
Kigoma. Shahidi wa 10 katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo ameieleza Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma kuwa uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kigoma ulipokea fedha kutoka kwa mbunge huyo kipindi cha uchaguzi.
Shahidi huyo Selemani Simba ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Bakwata ameeleza walipokea Sh3 milioni kutoka kwa Baba Levo.
Shahidi huyo, mkulima na mkazi wa Ujiji, Kata ya Kasingilima, ametoa maelezo hayo katika ushahidi wake wa maandishi uliopokewa mahakamani na kuwa sehemu ya ushahidi, leo Jumatano Julai 9, 2026.
Baba Levo alitangazwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda Zitto Kabwe wa ACT-Wazalendo na ushindi wake ukapingwa mahakamani na wapigakura wanne, Kabourou, Luma Akilimali, Pendo Kombolela, Lumu Mwitu na Johary.
Mbali na Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili, walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Walalamikaji hao wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za sheria na kanuni za uchaguzi na hivyo wanaiomba mahakama pamoja na mambo mengine, iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method kuhusu ushahidi wake wa maandishi, shahidi huyo amesema mgombea huyo alitoa fedha hizo Septemba 6, 2025.
Hata hivyo, amedai tukio hilo haliko kwenye hati ya walalamikaji.
Amesema ni kosa mgombea kutoa mchango kwenye shughuli za kidini kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, ingawa hajui ni kifungu gani cha sheria kinachokataza.
Katika maelezo yake ya ushahidi wa maandishi, pia ameandika kuwa Bakwata Mkoa wa Kigoma walipewa rushwa kwa mgongo wa mchango kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ni rushwa.
Alipoulizwa na wakili Vivian kama anakiri uongozi wa Bakwata mkoa ulipokea rushwa na una haki ya kushtakiwa, amejibu ndiyo ulipokea rushwa na una haki ya kushtakiwa.
Shahidi huyo katika mahojiano hayo amedai Baba Levo alitoa fedha hizo na akawaomba wamchague na kwamba wawaombe na waumini wao wamchague, jambo ambalo shahidi huyo amedai hiyo ni rushwa.
Shahidi huyo vilevile, ameeleza kuwa Oktoba 23, 2025 alipewa mwaliko wa kushiriki katika Kamati ya Maridhiano iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma katika ofisi yake ambako walipewa pesa kwenye bahasha.
Amefafanua pesa hizo alipewa Katibu Tawala wa wilaya ambaye ndiye aliyewagawia katika bahasha na alipoifungua bahasha hiyo akakuta pesa lakini yeye hakuichukua badala yake aliziicha kwenye kiti, kwa kuwa nafsi ilimwambia hiyo ni rushwa.
Alipoulizwa kama anakubali kwamba hajawasilisha ushahidi wowote mahakamani ukiwemo wa video, kuthibitisha madai yake, alikiri hana nyaraka ya uthibitisho huo.
Adai kutekwa
Shahidi huyo ameeleza siku ya Uchaguzi, Oktoba 29 alikamatwa na watu waliokuwa kwenye gari la polisi wakiwa wamefunika nyuso zao. Pia, walikuwa wamevaa sare za polisi na kwamba baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Ujiji, lilikuja gari lingine aina ya Land Cruiser na akachukuliwa na watu asiowajua.
Ameeleza tangu alipokamatwa aliachiwa huru siku iliyofuata saa tano asubuhi na alipoulizwa kama kwenye ushahidi wake ametaja namba ya gari hilo, amejibu hajazitaja.
Pia, amedai alipochukuliwa na polisi kwenda kituoni alikuwa amefungwa kitambaa machoni na kwamba tukio la kutekwa kwake liliratibiwa na Baba Levo, huku akifafanua kuwa alijua hilo kwa kuwa waliomteka walizungumza hivyo wakiwa kwenye gari.
Alipotakiwa kusoma alivyoandika katika maelezo yake, ilibainika hakuna mahali ameandika kuwa kutekwa kwake kuliratibiwa na Baba Levo, lakini akasisitiza ana uhakika vijana wale walitumwa na Baba Levo.
Alipoulizwa kama aliwahi kwenda kuripoti Kituo cha Polisi kuhusu tukio la kutekwa kwake Oktoba 29, 2025, amesema polisi hao ndio waliohusika kumteka, hivyo asingeweza kwenda kuripoti tena kwao.
Kwa mujibu wa maelezo yake, kutekwa kwake kulitia hofu kwa familia na majirani, hivyo wakashindwa kwenda kupiga kura. Alipoulizwa idadi ya hao walioshindwa kupiga kura kutokana na hofu hiyo, amejibu walikuwa takribani watu 26.
Hata hivyo, amejibu hakuwasilisha mahakamani majina ya hao walioshindwa kupiga kura wala vitambulisho vyao, kuthibitisha kama walikuwa na sifa ya kupiga kura.
Akisoma sehemu nyingine ya maelezo yake ya ushahidi wa maandishi, amedai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na kwamba uliingiliwa na watumishi wa umma, akiwemo Mkuu wa Wilaya, kwa kutoa rushwa na kumsaidia mgombea wa CCM dhidi ya mgombea wa ACT-Wazalendo.
Wakili wa Baba Levo
Akihojiwa na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa, shahidi huyo ameeleza ni mwanasiasa mzoefu na kiongozi wa ACT-Wazalendo akiwa mwenyekiti wa mkoa, na kwamba kwa sasa ni mwenyekiti wa Ngome ya Wazee ya ACT-Wazalendo.
Amedai katika uchaguzi wa mwaka 2025 hakushiriki katika kampeni kwa ajili ya mgombea wa ACT-Wazalendo, isipokuwa alimwombea kura kwa familia yake tu.
Alipoulizwa kama anakubali Bakwata haifanyi kosa kuomba michango kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, amesema haifanyi kosa.
Alipoulizwa kama anamfahamu Sheikh Mramba, amejibu ni mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo na akakiri kuwa ni mmoja wa viongozi wa dini wanaoheshimika.
Hata hivyo, alipoulizwa kama Sheikh Mramba ni mtu asiye na taswira ya kutiliwa shaka, amepinga akidai yeye ni binadamu tu na anaweza kutiliwa shaka, akasema ni malaika pekee wasiokuwa na taswira ya kutiliwa shaka.
Ameongeza kuwa hata yeye aliwahi kumtilia shaka Sheikh Mramba.
Alipoulizwa kuhusu fedha zilizotolewa na Baba Levo, kama alikabidhiwa yeye, amejibu hakukabidhiwa wala hakuzihesabu, lakini akasema baada ya kupokea fedha hizo walifanya dua na yeye alishiriki.
Hata hivyo, ameeleza hakuwahi kwenda kutoa taarifa za tukio hilo kwa viongozi wa dini wala katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Badala yake, ameeleza alilifikisha suala hilo katika Baraza la Bakwata, lakini halikuandikwa kwenye muhtasari kwa kuwa waliona ni aibu. Alipoulizwa kama aliwahi kuuona muhtasari huo, amejibu hajawahi kuuona wala hajauleta mahakamani.
Vilevile, amekiri hajawahi kuyataja mahakamani majina ya wanafamilia wake ambao walishindwa kupiga kura kwa hofu.
Akihojiwa na wakili John Seka anawawakilisha walalamikaji katika maswali ya kusawazisha, amesisitiza kuwa kupewa mchango wakati wa kampeni kwa sharti la kumchagua anayeutoa ni kosa.
Vilevile, akifafanua tukio la kutekwa kwake, ameeleza polisi ndiyo waliomkabidhi kwa watekaji, na ndio maana hakwenda kuripoti polisi kwa kuwa alijua katika mazingira hayo hangesaidiwa.
Pia, amefafanua kuwa akiwa kwenye gari la watekaji amefungwa kitambaa machoni, walikuwa wakimwambia, “Zitto wenu hatashinda, hapa ni Baba Levo tu,” na kwamba kauli hiyo ndiyo iliyomfanya aamini kuwa walitumwa na Baba Levo.
Endelea kufuatilia Mwananchi