Hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza katika shule za sekondari za amali imeendelea kuleta matumaini mapya kwa vijana nchini, huku ikitajwa kuwa suluhisho la changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu Nchini.
Kupitia shule 103 za amali zinazojengwa nchini, Serikali inalenga kuwajengea vijana ujuzi wa kujiajiri na kuajirika badala ya kutegemea ajira rasmi pekee ambapo miongoni mwa shule hizo ni Shule ya Sekondari ya Amali Ruvuma Juu mkoani Ruvuma, iliyoanza kupokea wanafunzi mwaka 2026. Serikali imewekeza shilingi bilioni 1.6 katika shule hiyo ambayo kwa sasa ina wanafunzi 172 wanaopata elimu ya kawaida ya sekondari sambamba na mafunzo ya ufundi stadi.
“Hii ni shule ya sekondari ya mkondo wa amali inayotoa elimu ya kawaida ya sekondari sambamba na mafunzo ya ufundi katika ufyetuaji wa tofali na ujenzi, usimikaji wa sola, chakula na lishe, kompyuta, sanaa ya kompyuta pamoja na ufundi bomba. Serikali imewekeza shilingi bilioni 1.6 kuhakikisha malengo ya shule yanafikiwa.” amesema Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Atemius Komba.
Kwa upande wao Wananchi wa Ruvuma Juu wanasema shule hiyo imefungua fursa mpya za elimu kwa vijana wa eneo hilo na kuongeza matumaini ya kujitegemea kupitia ujuzi wa vitendo ambapo Bi. Marry Haule, amesema mradi huo umeleta chachu kubwa kijijini kwao kwa kuwapatia vijana wao nafasi ya kupata elimu yenye ujuzi wa ziada.
Uwekezaji wa Rais Samia katika shule za amali ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana wanaohitimu masomo. Kupitia mfumo huu, vijana hawamalizi elimu wakiwa na matarajio ya kusubiri ajira pekee, bali wanakuwa na ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri, kuanzisha shughuli za uzalishaji na hata kuajiri wengine. Hatua hiyo inaendelea kuimarisha azma ya Rais Samia ya kujenga kizazi chenye uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
(Feed generated with FetchRSS)