
Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Usalama Barabarani limetoa siku 21 kwa wamiliki wa vyombo vya moto ambao bado hawajaingia kwenye mfumo wa Motor Vehicle Inspection Information System (MVIIS) na kukaguliwa vyombo vyao, kutumia muda uliosalia kutekeleza takwa hilo ili kuepuka changamoto za kisheria zitakazoanza baada ya Julai 30, 2026.
Hata hivyo, wadau mbalimbali, ikiwemo Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), wamesema pamoja na kuwapo kwa sheria hiyo, changamoto kubwa imekuwa ukosefu wa elimu ya kutosha kwa umma kuhusu utekelezaji wake.
Wameenda mbali na kuhoji iwapo Polisi wataweza kusajili vyombo vyote vya moto nchini kwa takribani wiki tatu pekee, wakisema Serikali inapaswa kuangalia hilo kwa makini ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza.
Julai 10, 2026, baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema muda wa mwisho wa kujiunga na mfumo huo ni Julai 30, 2026.
Alisema baada ya tarehe hiyo kuisha, operesheni maalumu ya ukaguzi itaanza nchini kote, na wamiliki wa vyombo vya moto watakaobainika kutotekeleza takwa hilo watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini.
“Baada ya muda huo, operesheni itaanza kwa kuwakagua wamiliki wa vyombo vya moto na kuwatoza faini ili kuhakikisha vyombo vyote vinakaguliwa kwa lengo la kusimamia usalama wa wananchi kupitia sheria za usalama barabarani,” alisema Ayoub.
Ayoub alisema kikao cha kamati hiyo kilifanyika baada ya tathmini kubaini kuwa baadhi ya maeneo nchini bado yanakabiliwa na changamoto kubwa za usalama barabarani, huku asilimia 46 ya ajali zikisababishwa na uzembe wa madereva.
Kutokana na hali hiyo, alisema kamati imeazimia kuendesha operesheni maalumu ya ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto nchini kwa kuzingatia Kanuni ya Nne ya Ukaguzi wa Lazima wa Vyombo vya Moto ya mwaka 2015, iliyotolewa kupitia Tangazo la Serikali la Januari 30, 2015, linalotaka kila chombo cha moto kikaguliwe angalau mara moja kwa mwaka.
Alisema tathmini ya baraza imeonyesha utekelezaji wa ukaguzi huo haujafanyika kwa kiwango kinachotarajiwa, hivyo Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limejipanga kusimamia kikamilifu utekelezaji wa kanuni hiyo ili kuhakikisha usalama wa wananchi unalindwa na ajali za barabarani zinapungua.
Mfumo wa MVIIS unalenga kuhakikisha vyombo vyote vya moto vilivyopo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinaingizwa kwenye mfumo kwa ajili ya ukaguzi wa lazima na usimamizi wa mamlaka husika, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usalama barabarani.
Mwananchi leo Jumapili, Julai 12, 2026, limezungumza na wadau mbalimbali kuhusu mfumo huo. Msemaji wa Taboa, Mustapha Mwalongo, amesema mamlaka husika zimekuwa zikitangaza utekelezaji wa sheria bila kwanza kuhakikisha wananchi wamepewa uelewa wa kutosha.
“Changamoto iliyopo ni mamlaka zinakurupuka kutoa matangazo bila kutekeleza wajibu wao wa kutoa elimu. Kama sheria ilitungwa, inashindwaje kutekelezwa? Kuna tatizo. Ukiniuliza, nitakwambia umma haupewi elimu ya kutosha, ndiyo maana utekelezaji wake hauwi wa mafanikio,” amesema Mwalongo.
Mkazi wa Morogoro, Mariam Ibrahim, anayemiliki gari, amesema yeye hakuwa anafahamu kuhusu kuanza kwa mfumo huo, huku akiomba Serikali kuwa makini kuanza kuchukua hatua, kwani uwezekano wa vyombo vyote kusajiliwa kwenye mfumo huo ni mdogo.
“Tuna magari mengi, pikipiki na bajaji, na elimu huku kwa kweli haipo. Watu wengi hawajui huu mfumo. Kilichopaswa kufanyika ni kuwekeza kwenye elimu kwa umma juu ya mfumo huu, lakini kulazimisha kupiga faini kwa ambao watakuwa bado hawajaingia, sijui, wacha tusubiri,” amesema Mariam.
Lilian Frank, mkazi wa jijini Dar es Salaam na mmiliki wa gari binafsi, amesema hafahamu kabisa mfumo huo na kwamba ndiyo kwanza ameusikia kupitia matangazo.
Amesema pia haelewi namna ya kujiunga na mfumo huo, akionya kuwa kutozwa faini bila kupewa elimu ya kutosha kutakuwa ni kuwaonea wananchi.
“Sijui kabisa mfumo huo; ndiyo kwanza nimesikia matangazo yao. Hata muda ukiisha na wakasema watutoze faini, itakuwa ni kutuonea kwa sababu tangu mwanzo tulikuwa tunalazimishwa kukata stika ya usalama barabarani, baadaye wakasitisha,” amesema.
Frank amesema wananchi wengi, akiwamo yeye, hawaufahamu mfumo huo na walipaswa kupewa elimu ya kutosha kabla ya Serikali kutoa matangazo ya utekelezaji wake.
Ameongeza kuwa, licha ya wengi kumiliki vyombo vya moto, bado hawana uelewa wa mfumo huo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Madogo na ya Kati Tanzania (TAMSTOA), Chuki Shabani, amesema yeye pamoja na wadau wake hawautambui mfumo huo na walishtushwa na tangazo la utekelezaji wake.
“Viongozi wetu wanakurupuka. Hakuna aliyekuwa anajua jambo hilo, wala hawajawahi kutuita kutuelimisha. Inashangaza Waziri anatokea mbele ya umma na kutoa tamko kama lile,” amesema.
Shabani amesema wakati tangazo hilo linatolewa, baadhi ya madereva wa malori walikuwa safarini kupitia Tunduma wakielekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kusafirisha mizigo, safari ambazo huchukua kati ya siku 45 na 60 kwenda na kurudi.
“Kilichotangazwa kinaweza kuleta mgogoro kwa sababu Tanzania si kisiwa. Hatukufikiwa wala viongozi wetu hawakushirikishwa ili waweze kutuelimisha. Hata kama kulikuwa na kamati, kamati hizo hazimiliki magari. Tatizo letu limekuwa ni kutegemea matamko kuliko ushirikishwaji,” amesema.
Ameongeza kuwa viongozi wa vyama vya usafirishaji wapo kwa ajili ya kuisaidia Serikali katika utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali, lakini wanashangazwa na kutoshirikishwa katika maamuzi yanayowagusa wadau wao.
Amesema vikao vingi hufanyika bila kuwashirikisha viongozi wa vyama vinavyowakilisha wamiliki wa vyombo vya moto, jambo linalochangia ukosefu wa uelewa na malalamiko miongoni mwa wananchi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Usalama Barabarani, William Mkonda, ambaye amepewa jukumu la kuratibu operesheni hiyo, aliwahimiza wamiliki wa vyombo vya moto na madereva kutumia muda uliosalia kuingia kwenye mfumo na kukamilisha ukaguzi wa vyombo vyao badala ya kusubiri operesheni ianze.
“Wasisubiri hadi operesheni ianze kwa sababu operesheni ina changamoto zake. Kusubiri ni kukubali kukabiliana na changamoto hizo. Tumiaeni muda uliobaki; ofisi za Makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani katika mikoa yote zinaendelea kutoa huduma hiyo na zimeainisha maeneo ya kufanyia ukaguzi,” alisema Mkonda.
Kuhusu malalamiko ya baadhi ya wananchi kudai kutouelewa mfumo huo, Mkonda amesema mfumo huo ni rahisi kuutumia na ulianza kufanya kazi mwaka jana baada ya kuzinduliwa rasmi Babati, mkoani Manyara.
Amesema baada ya uzinduzi huo, walifanya ziara katika mikoa mbalimbali kutoa elimu kwa makundi tofauti kuhusu namna ya kuutumia mfumo huo, ambao ni rahisi na rafiki kwa wamiliki wa vyombo vya moto.
“Tumepita katika mikoa mbalimbali kutoa elimu kwa makundi tofauti kuhusu namna ya kuutumia mfumo huu, ambao ni rahisi na rafiki kwa wenye vyombo vya moto. Ingawa jamii yetu imekuwa na tabia ya kutotaka kuelewa jambo hadi pale operesheni inapokuwa imeanza,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Mkonda amesema waliona ni muhimu kutoa muda wa kutosha kwa wadau kabla ya kuanza operesheni mwezi ujao, sambamba na kuongeza kasi ya utoaji wa matangazo ya uhamasishaji na kubainisha maeneo mengi zaidi ya ukaguzi.