New York, Marekani. Safari ya kuelekea ubingwa wa Kombe la Dunia 2026 sasa imebakiwa na mataifa manne makubwa ya soka duniani, huku kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo timu nne zinazoongoza viwango vya ubora duniani zikifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali.
Argentina, Hispania Ufaransa na England ndizo zimebaki kwenye mbio za kutwaa taji, jambo linaloweka mazingira ya kushuhudia mechi mbili zenye mvuto mkubwa na ushindani wa hali ya juu.
Katika nusu fainali, England itavaana na mabingwa watetezi Argentina, huku Hispania ikikabiliana na Ufaransa katika pambano jingine litakalozikutanisha timu mbili zinazocheza soka la kuvutia.
Hatua hii ya nne bora imeandika historia mpya ya Kombe la Dunia, kwani ni mara ya kwanza timu nne zinazoshika nafasi za juu kabisa kwenye viwango vya ubora vya FIFA zinakutana katika hatua ya nusu fainali.
Mashabiki wa soka duniani sasa wanasubiri kuona kama Lionel Messi ataendelea na safari ya kutetea taji lake au kama Jude Bellingham na England wataandika historia kwa kuiondoa Argentina.
Upande mwingine, macho yote yatakuwa kwa Kylian Mbappe na Ufaransa watakaokabiliana na Hispania ya Lamine Yamal inayocheza kwa kasi, pasi nyingi na nidhamu ya hali ya juu.
Kwa ubora wa vikosi vinne vilivyobaki, Kombe la Dunia 2026 linaelekea kumalizika kwa tamasha kubwa ambalo linaweza kuingia kwenye historia kama moja ya hatua bora zaidi za nusu fainali kuwahi kushuhudiwa katika soka la dunia.
Kinachoongeza hamasa ni uwezekano wa kushuhudia marudio ya fainali ya Kombe la Dunia 2022, kati ya Lionel Messi na Kylian Mbappe, endapo Argentina na Ufaransa zitafanikiwa kushinda mechi zao za nusu fainali.
Hata hivyo, kabla ya kufikiria fainali hiyo ya ndoto, Messi atalazimika kuiondoa England ya Harry Kane, huku Mbappe na wenzake wakikabiliwa na kazi ngumu dhidi ya Hispania ya Lamine Yamal inayocheza soka la kuvutia.
Argentina yaokoka dhidi ya Uswisi
Safari ya Argentina kuelekea hatua ya nne bora haikuwa nyepesi.
Katika robo fainali iliyochezwa Kansas City, kikosi cha Lionel Scaloni kilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Uswisi baada ya dakika za ziada.
Lionel Messi alionyesha ubora wake mapema kwa kumtengenezea Alexis Mac Allister bao la kuongoza ndani ya dakika 10 za mwanzo.
Lakini Uswisi ilisawazisha kupitia Dan Ndoye kipindi cha pili na kuifanya mechi kuwa ngumu.
Baada ya Breel Embolo kutolewa kwa kadi nyekundu, wengi walidhani Argentina ingeimaliza mapema mechi hiyo, lakini Uswisi iliendelea kupambana hadi dakika za nyongeza.
Hatimaye, Julian Alvarez aliifungia Argentina bao la pili dakika ya 112 kwa shuti la kuvutia, kabla ya Lautaro Martinez kufunga bao la tatu sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho na kuthibitisha ushindi.
England yaitoa Norway kwa jasho
England nayo ililazimika kufanya kazi ya ziada ili kuitoa Norway kwa ushindi wa mabao 2-1 baada ya dakika za nyongeza.
Baada ya kuiondoa Mexico katika hatua ya 16 Bora, kikosi cha Thomas Tuchel kilikutana na upinzani mkali kutoka Norway katika robo fainali iliyochezwa Miami.
Kwa mara nyingine, England ilionyesha uimara wa kiakili na kupambana hadi mwisho, ikifanikiwa kutinga nusu fainali na sasa inajiandaa kwa pambano la kihistoria dhidi ya Argentina jijini Atlanta.
Mchezo huo dhidi ya Norway haukukosa utata baada ya VAR kutumika kuchunguza kama mpira uligonga kamera maalumu ya juu ya uwanja (spider-cam) kabla ya England kusawazisha mabao.
Ufaransa na Hispania: Vita ya Ulaya
Upande mwingine wa ratiba, kutakuwa na vita kali kati ya mataifa mawili makubwa ya Ulaya.
Ufaransa ilitinga hatua hiyo baada ya kuichapa Morocco mabao 2-0 katika robo fainali iliyochezwa Boston.
Kikosi cha Didier Deschamps kilionyesha ukomavu kwa kutumia mashambulizi ya kushtukiza kuimaliza Morocco na kuendeleza ndoto ya kutwaa ubingwa.
Kwa upande wa Hispania, kikosi cha Luis de la Fuente kilifuzu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ubelgiji mjini Los Angeles.
Hispania ilitawala mchezo kwa pasi nyingi na umiliki wa mpira kabla ya kutumia nafasi chache ilizozipata kufunga mabao ya ushindi.
Hatua hii ya nusu fainali inaahidi kuwa miongoni mwa bora zaidi katika historia ya Kombe la Dunia, ikizikutanisha timu nne zenye ubora mkubwa, historia nzito na nyota wanaoweza kuamua mechi kwa muda wowote. Dunia sasa inasubiri kuona nani atafuzu kucheza fainali ya michuano mikubwa zaidi ya soka duniani.