Timu ya taifa ya soka ya Uhispania imefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Dunia la Fifa 2026 baada ya kuilaza Ufaransa kwa ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa mjini Dallas, Marekani.

Wakixheza kwa kujiamini wachezaji wa Uhispania walitawala mchezo huo na kuwafunika kabisa nyota wa timu ya soka ya Ufaransa Kylian Mbape na Osman Dembele. Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, Uhispania ilikuwa ikiongoza kwa bao moja kwa nunge lilipatikana katika dakika ya 22 ya mchezo kwa njia ya mkwaju wa penalty iliyopachikwa wavuni na Mikel Oyarzabal baada ya kinda machachari Lamine Yamal kuchezewa rafu katika eneo la hatari.

Kipindi cha pili Ufaransa iliingia uwanjani kwa kujitutumua ikijaribu kurejesha bao. Jahazi la Ufaransa lilizidi kuuzama katika dakika ya 58 ya mchezo baada ya Pedro Poro kupachika bao la pili na kuwaacha mashabiki wa Ufaransa wakiduwaa na kutoamini kilichokuwa kikitokea. Mchezo maridadi wa Uhispania uliwafunika kabisa wachezaji wa Ufaransa iliyokuuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe hilo kutokana na ukali wa safu yake ya ushambuliaji na kiwango cha mchezo walichokionyesha tangu mashindano hayo yalipoanza.

Ushindi huo umeiwezesha timu hiyo kufuzu kwa mara ya pili katika historia yake kucheza fainali ya Kombe la Dunia tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 2010.

Ushindi huo unaendeleza safari nzuri ya kocha Luis de la Fuente ambaye ameendelea kuiongoza Uhispania katika mafanikio makubwa kwenye mashindano ya kimataifa.

Timu hiyo sasa inasubiri mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Uingereza na Argentina mchezo ambao utachezwa leo ili kujua mpinzani wake katika fainali ya Julai 19.

Ndoto ya Ufaransa ya kucheza fainali ya tatu mfululizo ya Kombe la Dunia imefikia tamati na sasa watashuka dimbani kuwania nafasi ya nafasi ya tatu dhidi ya timu itakayopoteza nusu fainali ya leo. Je fainali itakuwa kati ya Uhispania na Argentina au Uhispania na Uingereza ambayo kwa mara ya mwisho ilitwaa kombe hilo mwaka 1966? Tusibiri dakika 90 za mchezo wa leo ndizo zitakazotupa jibu la swali hili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *