
Polisi ya Nigeria imemtia mbaroni mtu aliyeanzisha wakala bandia wa serikali uliokuwa ukifanyia kazi zake katika ofisi ya Rais kwa karibu miaka miwili.
Adeniyi Adeyemi Matthew alizuiliwa katika Jimbo la Osun, kusini-magharibi mwa Nigeria. Alikuwa akijitambulisha kama Mkurugenzi Mkuu wa “Baraza la Rais la Kukuza Uwekezaji wa Kigeni” (PFIPC).
Polisi walimtia mbaroni baada ya Mahakama Kuu ya Shirikisho katika Abuja kutoa kibali siku ya Jumanne.
Sakala hili limegonga vichwa vya habari nchini Nigeria tangu Rais Bola Tinubu alipoagiza kufanyika uchunguzi wa ufisadi dhidi ya taasisi hiyo wiki iliyopita.
Polisi ya Nigeria imesema kuwa maafisa kutoka Idara ya Ujasusi ya Jeshi na Timu ya Radiamali ya Intelijinsia ndio waliomtia nguvuyni Adeniy Adeyemi Mathewe. Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa makao makuu ya polisi mjini Abuja kwa mahojiano.
Ofisi ya Rais wa Nigeria imeeleza kuwa barua iliyoanzisha “Baraza la Rais la Kukuza Uwekezaji wa Kigeni” PFIPC ilikuwa ya kughushi. Uchunguzi wa kitaalamu wa polisi pia ulibaini kuwa saini ya Mkuu wa wafanyakazi wa Tinubu, Femi Gbajabiamila, iliyokuwemo kwenye barua ya uteuzi ilikuwa bandia.
Aidha imebainika kuwa, wakala huo ulikuwa na ofisi ndani ya Sekretariati ya Shirikisho huko Abuja; eneo ambalo kuna wizara nyingi za serikali.