Tanga. Halmashauri ya Jiji la Tanga imeanza rasmi kutekeleza mpango wa kuyaondoa mabasi yote yaendayo mikoani katikati ya jiji na kuyahamishia katika Stendi Kuu ya Mkoa iliyopo Kange, hatua iliyozua mvutano kati ya viongozi wa jiji, kampuni za mabasi na baadhi ya wananchi.

Wasafirishaji na abiria wanasema uamuzi huo umetangulizwa kabla ya kukamilika kwa makubaliano yaliyofikiwa kati yao na halmashauri kuhusu kuboresha huduma muhimu katika stendi hiyo mpya.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Mkoa wa Tanga (Taboa), Albert Peter, amesema Juni mwaka huu walikutana na viongozi wa Jiji waliowasilisha mpango wa kuhamisha mabasi kwenda Kange, lakini walikubaliana kwanza kukamilisha huduma muhimu kabla ya kuanza matumizi rasmi ya stendi hiyo.

Ametaja huduma hizo kuwa ni uwepo wa viti vya abiria, kituo cha polisi, zahanati, sehemu za chakula pamoja na maegesho ya daladala.

“Leo tumelazimishwa kuhamia Kange wakati makubaliano yote hayajatekelezwa. Hakuna viti vya abiria, hakuna kituo cha polisi wala huduma nyingine muhimu tulizokubaliana nazo,” amesema Albert.

Ameongeza kuwa Taboa haipingi matumizi ya Stendi ya Kange, bali inapendekeza mabasi yanayokidhi vigezo yaruhusiwe kupakia abiria katika ofisi zao zilizopo mjini huku yakipitia Kange kulipa ushuru wa Sh5,000 kwa siku hadi pale stendi itakapokamilika kwa asilimia zote.

Abiria wakihamishiwa kwenye basi jingine baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuzuiwa na askari wa Jiji la Tanga kwa kupakia abiria katika kituo kilichopo katikati ya jiji, kinyume na utaratibu mpya wa kuanzia safari katika Stendi Kuu ya Kange. Picha na Mbonea Herman.

Kwa upande wa abiria, nao walieleza kutoridhishwa na namna utekelezaji wa agizo hilo ulivyofanyika.

Msafiri Rashid Hassan amesema walijikuta wakipelekwa Kange bila kupewa taarifa za kutosha, jambo lililosababisha kuchelewa kwa safari na usumbufu mkubwa.

“Tulikaa kwa saa kadhaa bila kuelekezwa ratiba ya safari. Kama kulikuwa na mgogoro kati ya Jiji na wasafirishaji, sisi abiria hatukupaswa kubeba athari zake,” amesema.

Naye Esther Ngao amesema utaratibu mpya unaongeza gharama kwa wasafiri kutokana na kulazimika kutumia usafiri wa ziada kufika Kange badala ya kupanda mabasi katika maeneo ya karibu kama ilivyokuwa awali.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia mabasi ya Tashrif, Ratco, Abood na Royal Line yakizuiwa kuendelea na safari baada ya kukutwa yakipakia abiria mjini. Kila basi lilitozwa faini ya Sh250,000.

Mwanasheria wa Jiji la Tanga, Sebastian Banda, amesema mabasi hayo yalichukuliwa hatua kwa kukiuka agizo la Halmashauri la kupakia na kushusha abiria katika stendi ya Kange.

“Mabasi yote yaliyokaidi agizo yamepigwa faini ya Sh250,000. Yakishalipa kupitia control number tulizowapatia yataendelea na safari,” amesema Banda.

Akizungumzia suala hilo, Meya wa Jiji la Tanga, Mustapha Muhina maarufu Seleboss, amesema Halmashauri haijakurupuka katika utekelezaji huo.

Ameeleza kuwa awali walisitisha mpango huo kufuatia ushauri wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian. Hata hivyo, amesema Juni 12 mwaka huu walipokea barua kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi iliyowataka kusimamia matumizi ya vituo vikuu vya mabasi kwa mujibu wa sheria.

Muhina amesema kwa mujibu wa sheria za mipango miji vituo vya abiria vinapaswa kuanzia kituo cha Kange na kuendelea,  lakini sio katikati ya jiji la Tanga na kwa utaratibu huo sasa , safari zote za mabasi ya mikoani zinapaswa kuanzia katika Stendi Kuu ya Kange.

Aidha, ametangaza utaratibu wa mpito ambapo mabasi ya safari za alfajiri yataendelea kupakia abiria katika ofisi zao zilizopo mjini, huku yale yanayoondoka kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni yakitakiwa kuanzia safari zao katika Stendi ya Kange.

Amesema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa huduma za daladala kujiimarisha ili kurahisisha usafiri wa abiria kuelekea stendi hiyo mpya, huku Halmashauri ikiendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kuboresha huduma zinazohitajika.

Seleboss ameongeza kuwa hawakukurupuka kwenye uamuzi huo na wamezingatia  mahitaji ya wamiliki wa mabasi na abiria   licha ya kwamba wenye mabasi nao wanadai kwamba makubaliano yao ya awali hayakufikiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *