Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wahudumu zaidi wa afya wamegoma mjini Bunia, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakidai hawajalipwa mishahara yao.
Madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa mstari wa mbele walifunga lango la Hospitali Kuu ya Bunia wakisema wamekuwa wakipambana na mlipuko wa Ebola kwa miezi miwili na nusu bila malipo.
Mhudumu wa usafi hospitalini, Jeannine Anyie, amesema wanaendelea kuhatarisha maisha yao kwa kuwasaidia wagonjwa.
Mkazi wa Bunia, Denis Kpadjanga, amesema ni jambo la kusikitisha kuwaona wahudumu wa afya wakifanya kazi kubwa lakini hawajapata malipo yoyote.
Huu ni mgomo wa pili wa wahudumu wa afya ndani ya siku chache ambapo siku ya Jumatatu, wahudumu katika mji wa Rwampara pia walisitisha kazi wakitaka walipwe mishahara yao.
Mgomo huo unakuja wakati mlipuko wa Ebola ukiendelea kuongezeka. Hadi Jumatano, visa 2,011 vilikuwa vimethibitishwa, huku watu 754 wakifariki dunia. Wagonjwa 753 bado wanapatiwa matibabu au wako karantini, nao wengine 366 wamepona.
Wizara ya Afya imesema ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa umefikia asilimia 67 pekee, jambo linalozuia juhudi za kudhibiti maambukizi.
Mlipuko huo ulianza Mei 15 na unasababishwa na aina adimu ya virusi aina ya Bundibugyo. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema asilimia 80 ya visa vipya vinatokana na vyanzo vya maambukizi ambavyo bado havijafahamika.