Dar es Salaam. Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (Kakama), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), wamezindua ‘Mpango Elekezi wa Maandalizi na Mwitikio wa Majanga kwa Taasisi za Habari’ ukiwa na lengo la kuimarisha nafasi ya vyombo vya habari katika kuzuia na kukabiliana na majanga.

Mwongozo huo ulizinduliwa Bujumbura nchini Burundi Julai 7, 2026 na kutolewa ufafanuzi zaidi na Dk Caroline Asiimwe leo Alhamisi Julai 16, 2026  alipozungumza na Mwananchi.

Kwa mujibu wa Unesco, mwongozo huo umeandaliwa kwa kuzingatia Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Hatari za Majanga pamoja na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kupunguza Hatari za Majanga kwa ajili ya kujenga ustahimilivu wa jamii.

Unesco imeeleza kuwa huo ni mwongozo wa kwanza kuwahi kutolewa ukiwa na malengo ya kutoa mfumo wenye mapendekezo ya vitendo yatakayosaidia taasisi za habari kuandaa au kuboresha mipango yao ya kujiandaa na kukabiliana na majanga. Pia, kuimarisha ustahimilivu wa jamii kupitia utoaji wa taarifa sahihi kuhusu majanga zinazochochea mabadiliko ya tabia.

Shirika hilo limebainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi yamesababisha kuongezeka kwa majanga duniani, hali iliyovuruga maisha ya watu, kuharibu miundombinu na kuyaweka jamii nyingi katika hatari.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Majanga (UNDRR), zaidi ya Dola za Marekani 2.3 trilioni (takribani Sh6,210 trilioni) hupotea kila mwaka kutokana na majanga hayo.

UNDRR pia inaeleza kuwa ni asilimia 40 pekee ya nchi za Afrika zilizo na mifumo ya tahadhari za mapema inayoweza kushughulikia aina mbalimbali za majanga. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa nchi zenye mifumo hiyo zina kiwango cha vifo vinavyotokana na majanga kilicho chini mara nane ikilinganishwa na zile zisizo nayo.

Sura ya kitabu ambacho Kakama na Unesco wamezindua kwa ajili ya mwongozo kwa vyombo vya habari kushiriki kujikinga na majanga.

Aidha, hadi sasa nchi 32 za Afrika zimeanzisha mifumo ya kufuatilia na kurekodi hasara zitokanazo na majanga, ingawa Unesco inaeleza kuwa takwimu pekee hazitoshi kuokoa maisha bila kuzifikisha kwa wananchi kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dk Caroline Asiimwe alisema ili kujenga jamii zenye ustahimilivu ni muhimu kuziba pengo lililopo kati ya taarifa za kisayansi na hatua za wananchi kwa kushirikisha vyombo vya habari.

Alisema redio, televisheni, magazeti na majukwaa ya kidijitali vina nafasi muhimu katika kila hatua ya usimamizi wa majanga, kuanzia maandalizi hadi mwitikio.

“Barani Afrika, na hasa Afrika Mashariki, tumeshuhudia mchango mkubwa wa vyombo vya habari wakati wa majanga makubwa kama mafuriko, njaa na dharura za afya, ikiwamo janga la Uviko-19,” alisema Dk Asiimwe.

Aliongeza kuwa bila vyombo vya habari jamii nyingi zingekosa taarifa muhimu zinazoweza kuokoa maisha wakati wa dharura, licha ya vyombo hivyo pia kuathiriwa na majanga vinavyoripoti.

Hata hivyo, alisema vyombo vya habari bado vinaelemea kuripoti majanga baada ya kutokea badala ya kuwekeza katika maandalizi na uandishi unaojikita kwenye tathmini ya hatari na hatua za kinga.

Kwa mujibu wake, mwongozo huo utasaidia kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata taarifa sahihi na za kuaminika kabla, wakati na baada ya majanga, huku taasisi za habari zikiendelea kutekeleza wajibu wake hata zinapokumbwa na changamoto.

Alisema kutolewa kwa mwongozo huo kwa lugha ya Kiswahili kutarahisisha zaidi kufikisha maarifa hayo kwa wadau wengi katika Afrika Mashariki.

Kupitia maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika hivi karibuni, Kakama na Unesco zimeazimia kuufikisha mwongozo huo kwa vyombo vya habari ili kuviwezesha kuimarisha mipango yao ya ndani pamoja na mifumo ya pamoja ya sekta ya habari katika maandalizi na mwitikio wa majanga.

Hatua hiyo imewezekana baada ya kutafsiri chapisho hilo kwa Kiswahili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuanzisha mijadala inayozingatia mazingira na mahitaji ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na jumuiya ya wanasayansi.

Dk Asiimwe alisema mwongozo huo utasaidia kutafsiri maarifa na takwimu za kisayansi katika lugha rahisi inayoweza kueleweka na kuchochea hatua za serikali pamoja na jamii.

Pia, alivitaka vyombo vya habari kuutumia mwongozo huo kama sehemu ya mikakati ya kujilinda dhidi ya athari za kiuchumi zinazoweza kusababishwa na maandalizi duni ya kukabiliana na majanga, huku akivitaka kuhakikisha vinaendelea kuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa umma wakati wa dharura.

Dk Asiimwe aliipongeza Unesco na wadau wote waliohusika katika maandalizi ya chapisho hilo, akisema lengo lake ni kujenga jamii zenye ustahimilivu, zenye taarifa sahihi na zinazoweza kuelewa pamoja na kushiriki mijadala ya kimataifa kwa kutumia lugha zao wenyewe, hususan Kiswahili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *