Marekani. Mwimbaji wa muziki wa R&B, R. Kelly, amewasilisha ombi kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, akiomba apunguziwe kifungo chake cha miaka 31 jela alichopewa baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya uhalifu wa kupangwa (racketeering), biashara ya ngono na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 59, ambaye jina lake halisi ni Robert Sylvester Kelly, alipatikana na hatia mwaka 2021 kwa kuongoza mtandao wa kihalifu uliowashawishi wanawake na wasichana walio chini ya umri kushiriki vitendo haramu vya ngono pamoja na utengenezaji wa picha za ponografia za watoto. Kutokana na makosa hayo, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Mwaka 2022, R. Kelly alipatikana tena na hatia katika makosa matatu ya kutengeneza picha za unyanyasaji wa watoto na makosa matatu ya kuwashawishi watoto kwa nia ya kingono. Alihukumiwa kifungo cha miaka 20, lakini sehemu kubwa ya kifungo hicho inatumikia sambamba na kile cha awali, hivyo kufanya jumla ya kifungo anachotumikia kuwa miaka 31.

Kwa sasa, anatumikia kifungo hicho katika gereza la shirikisho lililopo jimbo la North Carolina, huku akitarajiwa kumaliza adhabu yake mwezi Januari 2046.

Ombi lake la kupunguziwa kifungo limefichuliwa kupitia nyaraka za mahakama zilizowekwa wazi wiki hii na Ofisi ya Mwanasheria wa Masuala ya Msamaha (Office of the Pardon Attorney), ambayo hupokea na kupitia maombi ya msamaha au kupunguziwa adhabu kabla ya kuyawasilisha Ikulu ya White House.

Wakili wa R. Kelly, Beau Brindley, amekuwa akimshawishi hadharani Rais Trump kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kulingana na nyaraka hizo, ombi hilo bado linaendelea kufanyiwa kazi (pending) na si ombi la msamaha kamili, bali ni la kupunguziwa kifungo.

Hii si mara ya kwanza kwa Brindley kuwasilisha ombi kama hilo. Mwaka 2025, aliwasilisha ombi la dharura mahakamani akiomba mteja wake aachiliwe kutoka gerezani na kuwekwa kifungo cha nyumbani, akidai kuwa maisha ya R. Kelly yalikuwa hatarini.

Brindley alidai kuwa maafisa watatu wa gereza walipanga njama za kumtumia mfungwa mwenye ugonjwa usiotibika kumuua R. Kelly kwa ahadi ya kuachiwa huru mapema.

“Kitu pekee kinachoweza kumlinda R. Kelly akiwa gerezani kwa sasa ni ukweli kwamba dunia nzima sasa inafuatilia kinachoendelea. Tutaendelea kuziomba mahakama na Rais Trump kusaidia kukomesha ufisadi ambao sasa unatishia maisha ya Kelly,” alisema Brindley.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *