Shinyanga. Katika jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza ajali za barabarani zinazochangiwa na makosa ya kibinadamu, Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) Mkoa wa Shinyanga kimeanza kutoa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wakufunzi wa vyuo vya udereva kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi.
Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha ubora wa ufundishaji ili kuzalisha madereva wenye taaluma, maadili na uelewa mpana wa sheria za usalama barabarani.
Hatua hiyo imekuja wakati ajali za barabarani zikiendelea kuwa changamoto nchini, huku nyingi zikichangiwa na makosa ya kibinadamu, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na uelewa mdogo wa baadhi ya madereva kuhusu matumizi salama ya barabara.
Akizungumza leo Julai 16, 2026, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Veta Shinyanga, Rashid Ntahigiye amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Veta wa kuboresha ubora wa mafunzo ya udereva nchini kwa kuanza na kuwajengea uwezo wakufunzi, ambao ndiyo msingi wa kuzalisha madereva wenye weledi.
Amesema Veta itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazohusika na usalama barabarani ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
“Lengo letu ni kuhakikisha wakufunzi wa vyuo vya udereva wanakuwa na viwango vinavyofanana vya kitaaluma, ili madereva wanaohitimu wawe na uwezo wa kuendesha vyombo vya moto kwa usalama na hivyo kuchangia kupunguza ajali za barabarani,” alisema Ntahigiye.
Kaimu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga, Rashid Ntahigiye akizungumza kuhusu hatua mpya ya kupunguza ajali za barabarani. Picha na Hellen Mdinda
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema wakufunzi ndiyo msingi wa kuzalisha madereva bora, hivyo kuwajengea uwezo kutasaidia kupunguza ajali zinazotokana na uzembe, mwendo kasi, matumizi yasiyo sahihi ya sheria za barabarani na maamuzi yasiyofaa yanayofanywa na baadhi ya madereva.
Mkufunzi wa udereva kutoka Veta Shinyanga, Axivier Msolla, amesema mafunzo hayo yamewapa fursa ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mpya za ufundishaji zinazokidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya usafiri na usalama barabarani.
“Mafunzo haya yanatuwezesha kuboresha mbinu za kufundisha ili kuandaa madereva wenye ujuzi unaoendana na mazingira ya sasa ya matumizi ya barabara,” alisema Msolla.
Kwa upande wao, wakufunzi kutoka Tabora na Biharamulo, Athuman Mohammed na Jekonia Shedrack wamesema maarifa waliyopata yatawawezesha kuongeza ubora wa mafunzo wanayotoa katika vyuo vyao.
Walisema hatua hiyo itachangia kuzalisha madereva wenye ujuzi, nidhamu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanapokuwa barabarani, jambo litakalosaidia kupunguza ajali na kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.