KILA shabiki wa Yanga anasubiri kuona mziki wa kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao utakuwaje, sasa imejulikana siku ambayo shughuli ya kuanza kushusha silaha zao.

Yanga imetanganza kazi ya kuanza kutengeneza kikosi cha msimu ujao itaanza Jumatatu Julai 20, 2026 kwa timu hiyo kukutana, ikiwa ni siku tatu zimebaki kutoka leo Ijumaa Julai 17, 2026.

Siku tatu kabla ya kuanza balaa hilo, kocha mpya wa Yanga, Manqoba Mngqithi, alitarajiwa kuwasili nchini usiku wa jana Alhamisi akitokea kwao Afrika Kusini, tayari kwa kuanza majukumu yake mapya na klabu hiyo.

Mnqithi anawasili na wasaidizi wake watatu kwenda kuunda benchi lake jipya la ufundi, akiungana na wengine ambao ameamua kuwabakisha kutoka kwenye benchi lililopita.

Yanga haitatoka nje ya nchi kwa sasa baada ya kufeli kwa mpango wa kwenda Afrika Kusini kushiriki mashindano ya Toyota.

Baada ya kufeli kwa safari hiyo, Yanga itaweka kambi yake palepale kwenye kiota chao cha Avic Town kilichopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam, ambako kumefanyiwa marekebisho makubwa.

Yanga ina rekodi nzuri na maandalizi yao pale Avic Town na imewahi kukaa hapo kwa mazoezi ya mwanzo wa msimu na kuchukua mataji mara tatu kati ya rekodi ya mataji matano mfululizo.

Hapo Avic Town, Mwanaspoti linafahamu gym ya kisasa imeimarishwa ambayo itatumiwa kwa mazoezi ya awali na kabla, kikosi cha Yanga kilikuwa kikienda kujifua pale viwanja vya Gymkhana.

ULINZI MKALI

Yanga imejipanga kambi hiyo itakuwa na ulinzi mkali kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kushuhudia mazoezi ya kikosi hicho, zaidi ya viongozi wao pekee.

“Haitakuwa rahisi kufika pale na kuona mazoezi nje ya viongozi wa klabu, yaani pale kuna ulinzi lakini utaongezwa zaidi, watu watakuja kujionea kikosi chao uwanjani,” amesema bosi mmoja wa juu wa Yanga.

Yanga pia imepanga kuhakikisha hata mechi za kirafiki za kujipima nguvu zitachezwa huko huko kambini kwao katika kuhakikisha hakuna taarifa za mipango yao zikivuja.

Yanga inaanza maandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-2027 ikiwa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu ya NBC, hivyo itafungua msimu kwa kucheza dhidi ya Simba, Agosti 12, 2026 ikiwa ni mechi ya Ngao ya Jamii.

Wakati Yanga ikisalia Dar es Salaam kujiandaa na msimu ujao, Jumamosi ya Julai 18, 2026, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuingia kambini tayari kwa maandalizi ya kwenda Rwanda kushiriki Kombe la Kagame, michuano inayoanza Julai 24 hadi Agosti 7, mwaka huu ikishirikisha timu 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *