SIMULIZI ya kusikitisha ya aliyekuwa kiungo wa Mbao FC na Serengeti Boys, Lipston Mlagulwa, imegusa mioyo ya wadau mbalimbali wa soka huku nyota wa Taifa Stars, Simon Msuva akiwa miongoni mwa walioamua kuchukua hatua kufuatia kile ambacho Mwanaspoti iliripoti.
Lipston ambaye kwa sasa hawezi kutembea baada ya kupoteza nguvu za mwili kutokana na tatizo ambalo bado halijapatiwa ufumbuzi wake licha ya kupitia hospitali mbalimbali, katika mahojiano yake na Mwanaspoti alimtaja Msuva kuwa mmoja wa wachezaji wa Kitanzania aliokuwa akiwapenda na kuwatazama kama mfano wa mafanikio katika soka.
Kauli hiyo ilimgusa Msuva ambaye kwa sasa amesaini kuichezea Newroz FC ya Iraq akitokea Al-Talaba SC ya nchini humo, baada ya kumaliza mapumziko yake nchini Tanzania. Mara baada ya kusikia sakata la mchezaji huyo hakusita kufanya naye mawasiliano ili kumpa pole na kumtia moyo.
Katika mazungumzo yao, Msuva alimweleza Lipston kuwa asikate tamaa licha ya changamoto kubwa anayopitia, akisisitiza kuwa bado anaamini ipo siku mambo yatabadilika na afya yake itaimarika endapo ataendelea kupambana na kupata msaada unaohitajika.
Mbali na kumpa maneno ya faraja, nyota huyo wa Taifa Stars alimwahidi kumshika mkono huku akisema atashirikiana na wadau wengine kuhakikisha kijana huyo hapotezi matumaini katika safari yake ya kutafuta matibabu.
Hatua ya Msuva imeonekana kuwa mwanzo wa mwamko mpya wa wadau wa soka nchini, wengi wakiamini kuwa ushirikiano wa wachezaji, viongozi na mashabiki unaweza kuwa sehemu ya kumrejeshea matumaini kijana huyo ambaye miaka michache iliyopita alikuwa na ndoto za kuvaa jezi ya Taifa Stars.
Kwa upande wake, Lipston amesema simu ya Msuva imempa nguvu mpya na kumfanya ahisi kuwa bado hajasahaulika na familia ya soka la Tanzania, jambo ambalo limempa faraja kubwa wakati huu mgumu wa maisha yake.
“Nimefarijika sana. Sikutarajia kama ningeongea naye. Amenipa moyo mkubwa na kuniahidi kuwa pamoja nami. Namshukuru sana kwa upendo aliounionesha,” amesema Lipston.
Ameongeza kuwa, msaada wa Msuva unapaswa kuwa chachu kwa wadau wengine wa michezo kujitokeza, akisisitiza kuwa bado anaamini anaweza kupata nafuu ikiwa atapata matibabu sahihi na programu maalumu za kurejesha nguvu za mwili.
“Ninaomba wadau wengine pia wajitokeze. Naamini Mungu anaweza kutumia mtu yeyote kunisaidia kufikia hatua ya kupata matibabu yatakayobadilisha maisha yangu,” amesema kwa matumaini.
Kwa mujibu wa daktari bingwa wa mifupa, Dk. Shadrack Faustine, hali kama anayopitia Lipston haiwezi kutolewa hitimisho kwa kuangalia vipimo vya kawaida pekee, kwani kupoteza uwezo wa kutembea kunaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali yanayohusisha mfumo wa fahamu, uti wa mgongo, misuli au mishipa ya fahamu.
Dk. Faustine alieleza kuwa, mgonjwa wa aina hiyo anahitaji uchunguzi wa kina unaoweza kujumuisha vipimo maalumu kama MRI au CT Scan pamoja na tathmini ya wataalamu wa mfumo wa fahamu, mifupa na tiba mazoezi (physiotherapy), ili kubaini chanzo halisi kabla ya kuanza matibabu yanayolenga tatizo husika.
Alisisitiza kuwa, hata kama vipimo vya awali vinaweza kuonyesha hakuna tatizo kubwa, bado mgonjwa anaweza kuendelea kupata changamoto, hivyo uchunguzi wa kina ndio unaoweza kutoa mwanga wa tiba sahihi na kuongeza nafasi ya kupata nafuu.
Kwa sasa, matumaini ya Lipston hayapo tena katika kurejea uwanjani kama ilivyokuwa ndoto yake ya awali, bali ni kuona anarudi kusimama na kutembea tena kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita.