Chanzo cha picha, alarmy
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4
Aprili 7, 1989, moto mkubwa ulitokea katika sehemu ya nyambizi ya Komsomolets ilipokuwa ikifanya kazi katika kina cha maji cha takriban mita 335 (futi 1,100) katika Bahari ya Norway.
Nyambizi hiyo ilikuwa moja ya kazi bora ya uhandisi wa Kisovieti, ilikuwa na umbo la kipekee na nguvu, ikiiruhusu kuzama mbali zaidi kuliko karibu chombo kingine chochote cha nchi za Magharibi.
Wafanyakazi walifanikiwa kuileta juu nyambizi hiyo, na ilibaki ikielea kwa saa tano huku mabaharia wakipambana na moto. Hata hivyo, uharibifu ulikuwa mkubwa sana. Nyambizi hiyo hatimaye ilizama hadi kina cha karibu mita 1,700 (kama maili 1).
Kati ya wafanyakazi 69 waliokuwa ndani ya meli, 42 waliangamia. Wengi walikufa kutokana na baridi katika maji ya Aktiki yenye baridi kali walipokuwa wakisubiri kuokolewa, na wengine walinaswa ndani ya nyambizi.
Nyambizi ilipotua chini ya bahari, nyambizi ndogo ya dharura ilifanikiwa kung’oa nanga, ikiwaleta juu ya maji mabaharia watano walionaswa katika nyambizi, ingawa ni mmoja tu aliyepona na kutoka.
Bomu la chini ya bahari
Baada ya kugonga sakafu ya bahari, nyambizi hiyo ililipuka na kuisambaratisha. Mpasuko huu uliweka wazi shehena ya nyuklia ya chombo hicho moja kwa moja kwenye mazingira ya baharini.
Kulikuwa na mafuta ya urani yaliyorutubishwa na topido mbili zenye vichwa vya nyuklia zilizobeba takriban pauni 9 (kilo 4) za plutonium-239 yenye sumu kali.
Mwaka 1993, mwanaharakati wa mazingira wa Urusi, Dimitri Litvinov alionya katika ripoti kwamba ajali hiyo ni bomu linalosubiri kulipuka chini ya Bahari ya Norway.
Wakati huo, wanasayansi walitabiri kwamba maji ya chumvi yataharibu kabisa maganda ya vichwa vya nyuklia ndani ya muongo mmoja, na kufanya sumu ya plutonium kuingia baharini.
Ili kuzuia janga kubwa la ikolojia, wahandisi wa baharini wa Urusi na kimataifa walianza mfululizo wa misheni hatari sana kati ya 1994 na 1996.
Kwa kutumia nyambizi waliweza kufunga nyufa kwenye sehemu ya mbele ya nyambizi, kuchomeka mirija kwenye topido ili kupunguza mgusano wa maji ya bahari na vichwa vya nyukilia na kuweka vifungashio maalum vya kemikali vilivyoundwa kunyonya au kuzuia uvujaji wa mionzi.
Hata hivyo, mkakati huu wa kuzuia nyuklia kueneo ulikuwa na kasoro zake. Vifungashio vilibuniwa kudumu kwa miaka 30 tu, na miaka hiyo tayari imetimia Julai 2026.
Tishio la leo
Chanzo cha picha, thebarentsobserve
Ufuatiliaji wa hivi karibuni uliofanywa na Mamlaka ya Usalama wa Mionzi na Nyuklia ya Norway (DSA) unathibitisha kwamba Komsomolets inavujisha mionzi ya cesium-137, huku kiwango cha mionzi hiyo kikifikia mara 800,000 zaidi ya viwango vya kawaida vya mionzi vinavyohitajika chini ya bahari.
Licha ya idadi hii ya kutisha, wataalamu wanahimiza utulivu badala ya hofu. Maafisa wanabainisha kuwa: Kina kikubwa cha mita 1,700 na kiasi kikubwa cha maji ya Aktiki hupunguza kiwango cha mionzi haraka, na kufanya tishio kwa uvuvi na afya ya binadamu kuwa dogo.
Kuharibu mafuta ya nyuklia na vichwa vya nyuklia ni jambo lenye changamano sana, chini ya mikondo ya bahari ya kina kirefu na athari za kielektroniki ambazo wanasayansi bado wanajaribu kuzichorea ramani.
“Mafuta ya nyuklia yanagusana moja kwa moja na maji ya bahari na hali inazidi kuwa mbaya,” anaonya Ingar Amundsen mkurugenzi wa Taasisi ya kimataifa ya usalama wa nyukulia, DSA, akisisitiza kwamba utafiti zaidi unahitajika haraka ili kuelewa uchafuzi huu.
Vizuizi vya kijiografia
Licha ya hitaji dhahiri la ufuatiliaji na ulazima wa kuziba tena, hatua zaidi zimekwama kwa sasa. Uhusiano wa kijiografia na kisiasa uliozorota kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi, hasa Norway umezuia safari za pamoja za mazingira katika Aktiki.
Kwa kuwa kifungashio cha awali cha miaka 30 kinaisha rasmi na hakuna safari za pamoja ukaguzi, Komsomolets inasalia kuwa kumbukumbu ya Vita Baridi, ikisubiri suluhisho kabla ya kizuizi chake kuharibika kabisa.