WAKATI Simba SC ikianza maandalizi ya msimu mpya, matumaini mapya yameanza kuibuka baada ya mabeki wa kati Abdulrazack Hamza na Wilson Nangu kuanza hatua za kurejea uwanjani baada ya kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na majeraha tofauti hali ambayo inaonyesha kuwa sasa kuna ugumu wa namba kwenye timu hiyo.

Hali za wachezaji hao zimekuwa zikifuatiliwa kwa karibu huku daktari wa kikosi hicho, Edwin Kagabo akieleza kuwa wote wawili walikuwa miongoni mwa wachezaji waliopata majeraha yaliyohitaji muda mrefu wa matibabu na uangalizi mkubwa kabla ya kurudi kwenye ushindani.

Kwa mujibu wa daktari huyo, Hamza alipata jeraha kubwa la goti ambalo lilihitaji kufanyiwa upasuaji, jambo lililomuweka nje kwa sehemu kubwa ya msimu uliopita. Hata hivyo, baada ya kukamilisha hatua mbalimbali za matibabu, sasa ameanza mazoezi mepesi ya uwanjani.

“Hamza tulianza naye msimu uliopita lakini alipata changamoto kwenye goti ambalo lilihitaji upasuaji. Baada ya matibabu yake sasa tunaendelea kufuatilia hatua kwa hatua kuhakikisha anarudi akiwa salama na mwenye uwezo wa kushindana,” amesema daktari Edwin.

Kwa upande wa Nangu, daktari huyo alieleza kuwa jeraha lake lilikuwa tofauti na la Hamza baada ya kuumia kifundo cha mguu (Achilles tendon), aina ya majeraha ambayo yanahitaji uvumilivu mkubwa kutokana na muda wa kupona na hatari ya kujirudia.

“Nangu alipata jeraha la ‘tendon’ ambalo lilihitaji upasuaji. Haya ni majeraha ambayo huwezi kuyaharakisha kwa sababu unahitaji kuhakikisha nguvu, uwezo wa kukimbia na utayari wa mchezaji vinarudi vizuri kabla ya kumrudisha kwenye ushindani,” ameongeza Edwin.

Kwa mtazamo wa kitabibu, kurejea kwa Hamza na Nangu hakutegemei tu kupona kwa jeraha, bali pia uwezo wao wa kurejesha kiwango cha juu cha ushindani. Kwa kawaida, mchezaji anayetoka kwenye upasuaji wa goti anaweza kuhitaji miezi tisa hadi 12 kabla ya kurudi kwenye mechi za ushindani huku majeraha ya ‘Achilles tendon’ yakihitaji uangalizi mkubwa zaidi.

Hivyo, hatua ya kuanza mazoezi mepesi haimaanishi moja kwa moja kuwa wachezaji hao wako tayari kucheza mechi rasmi, bali ni sehemu ya mchakato wa kuwarudisha kwenye kiwango ambacho hakitawaweka kwenye hatari ya kupata majeraha mapya.

Lakini kurejea kwao kunakuja na sura nyingine muhimu ndani ya kikosi cha Simba, hasa kwenye eneo la beki ya kati ambalo msimu uliopita lilikuwa na ushindani mkubwa. Simba ilikuwa na mabeki wanne wa kati ambao walitumika katika mazingira tofauti huku Rushine De Reuck na Ismail Toure  wakiwa ndio waliopata nafasi kubwa zaidi.

Mbali na Rushine na Toure, Simba pia ilikuwa na Yahya Mbegu pamoja na Vedastus Masinde ambao walikuwa sehemu ya mipango ya kikosi hicho, lakini hawakuwa na nafasi kubwa ya kucheza mara kwa mara ukilinganisha na wenzao wawili waliokuwa wakitumika zaidi.

Endapo Hamza na Nangu watakuwa tayari kuanza kutumika baada ya miezi miwili hadi mitatu ijayo, benchi la ufundi la Simba litajikuta likiwa na chaguo nyingi zaidi kwenye eneo hilo, jambo litakaloongeza ushindani wa namba na kutoa changamoto kwa kila beki kuhakikisha anabaki kwenye kiwango cha juu.

Kwa upande wa kocha, kuwa na mabeki wengi wenye uwezo tofauti ni faida kubwa hasa katika msimu wenye mashindano mengi, kwani inampa nafasi ya kubadilisha mifumo na kutumia wachezaji kulingana na aina ya mpinzani.

Hamza anajulikana kwa uwezo wake wa kusoma mchezo, nguvu kwenye mipira ya juu na utulivu akiwa na mpira, wakati Nangu naye amekuwa akionekana kuwa na uwezo wa kucheza kwa nguvu na kusaidia timu kwenye mapambano ya moja kwa moja.

Hata hivyo, jambo la msingi kwa Simba litakuwa kuhakikisha hakuna presha ya kuwarudisha mapema wachezaji hao kwa sababu ya ushindani wa nafasi. Kama daktari Edwin alivyoeleza, majeraha makubwa yanahitaji mpango maalumu na kila hatua lazima ifuatwe kwa umakini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *