
Habari za Iran na Marekani ni kizunguzungu kwa sasa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, anasema kuna mpango wa amani. Muda mfupi unaofuata, bosi wake, Rais Donald Trump, anatangaza mashambulizi ya kisasi dhidi ya Iran.
Upande mmoja unaelezwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amekwenda Pakistan kwenye mazungumzo ya amani, wakati huohuo, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, anasema mashambulizi ya Marekani ndani ya Iran sasa yamechokoza vita kamili.
Ripoti mpya zinasema wanajeshi 17 wa Marekani wameuawa, na zaidi ya 427 wamejeruhiwa, kutokana na mashambulizi ya Iran kwenye ngome za Marekani Mashariki ya Kati. Trump anasema Iran lazima ilipe gharama za vifo vya wanajeshi hao waliokufa kishujaa wakati wakipambana kuidhibiti nchi hiyo ya Uajemi kumiliki silaha za nyuklia.
Iran wameripoti mashambulizi makali yaliyofanywa dhidi yao kwenye mji wa Bandar Abbas, uliopo Mkoa wa Hormozgan. Bandar Abbas ni bandari kubwa kabisa ya Iran kwenye Mlango Bahari wa Hormuz. Mashambulizi mengine makali ya Marekani yanatekelezwa kwenye mji wa Sirik, uliopo pwani ya Bahari ya Oman, upande wa Iran.
Dunia hivi sasa inatikiswa kiuchumi kutokana na uamuzi wa Iran kudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz. Mkwamo zaidi wa kibiashara unatarajiwa kuongezeka, kufuatia kikundi cha Houthis kutangaza kuufunga Mlango Bahari wa Bab el Mandeb.
Houthis, jina rasmi ni Ansar Allah, yaani Wenye Nusura ya Mwenyezi Mungu. Kikundi hiki ni jamii ya madhehebu ya Zaydi Shia, na kinaungwa mkono na Ira. Kwa sasa Houthis ndiyi wananadhibiti eneo lote la Kaskazini ya Yemen, ikiwamo mji mkuu wa nchi hiyo, Sanaa.
Hivi karibuni, Saudi Arabia, ilifanya mashambuzi ya anga kwenye Uwanja wa Ndege wa Sanaa. Serikali ya Saudi ilisema ilifanya hivyo ili kudhibiti ndege ya Iran kutua Yemen. Serikali ya Tehran, ilitoa ufafanuzi kuwa ndege yao ilikuwa imewapeleka maofisa wa Yemen, waliotoka kuhudhuria mazishi ya Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi mkuu wa Iran, aliyeuawa Februari 28, 2026, siku ya kwanza ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Kitendo cha Saudi kushambulia Uwanja wa Ndege wa Sanaa, kimeamsha hasira za Houthis, ambao wanasema wanaweka udhibiti majini.
Tangu mwaka 2014, Houthis walipoudhibiti mji mkuu wa Sanaa, Saudi walidhibiti njia za maji ili kuhakikisha safari za kibiashara haziathiriki.
Tamko la Houthis kuwa wanaanza kuidhibiti Saudi katika makabiliano ya “jicho kwa jicho”, maana yake hatari kubwa inakwenda kutokea. Hivi sasa, bei ya nishati imepanda kutokana na kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz. Nini kinakwenda kutokea kwa mlango mwingine kuzibwa?
Yemen ipo kwenye Mlango Bahari wa Bab el Mandeb, ambao ni lango la Kusini la Bahari ya Shamu. Uamuzi wowote wa kuufunga mlango bahari huo, utaibua mtikisiko mkubwa wa uchumi, utasababisha gharama ya nishati duniani kote ipande.
Pamoja na hivyo, msemaji wa Houthis, Yahya Saree, anasema lazima kuweka vizuizi baharini ili kukabiliana na vikosi vya Saudi.
Ufafanuzi zaidi kuhusu Bab el Mandeb ni kuwa mlango bahari huo ni kiunganisha kati ya Bahari ya Sham na Bahari ya Arabuni, ambayo ni sehemu ya Bahari ya Hindi. Bab al Mandeb pia huwezesha meli kupita kutokea Mfereji wa Suez. Kwa kifupi, Bab el Mandeb ni moja ya njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa bidhaa baharini, hasa mafuta ghafi kutoka Ghuba ya Uarabuni yakielekezwa Bahari ya Mediterania.
Upana wa Bab el Mandeb ni karibu sawa na Hormuz, kwa hiyo inakuwa rahisi kuudhibiti. Mandeb upana wake ni maili 20 (kilometa 32), wakati Hormuz ni maili 21 (kilometa 33.8).
Hii ndiyo hatari. Kwamba kama ilivyowezekana kwa Iran kuifunga Hormuz dhidi ya Marekani, haishindikani kwa Houthis Bab el Mandeb dhidi ya Saudi Arabia.
Asilimia 25 ya shehena za mizigo yote ulimwenguni, hukatiza kwenye Mlango Bahari wa Bab el Mandeb kuelekea au kutokea Mfereji wa Suez.
Ifahamike asilimia 12 ya thamani ya biashara yote ulimwenguni, hupitia Mfereji wa Suez. Zaidi, Bab el Mandeb, ni njia kuu ya Saudi Arabia kupitisha mafuta ghafi yake.
Upande wa Hormuz, asilimia 25 ya mafuta ghafi kwenda soko la dunia, hupitia Hormuz. Ni wastani wa mapipa milioni 20 mpaka 25 kwa siku.
Meli kubwa za kusafirisha mafuta, zisizopungua 14, hupita Hormuz zikiwa na shehena za mafuta na gesi asilia (LNG), kuelekea soko la dunia.
Katika jiografia ya dunia, Hormuz ni mlango bahari unaounganisha maji baina ya Ghuba ya Uajemi (Ghuba ya Arabuni) na Ghuba ya Oman (Bahari ya Makran).
Mlango bahari huo unahusisha pia mkondo muhimu unaounganisha maji ya Bahari ya Arabuni na Bahari ya Hindi, vilevile huzitenganisha nchi za Iran (upande wa Kaskazini), halafu Kusini zipo Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Ukiifuata ramani ya Hormuz kutokea Ghuba ya Oman, nchi ya Pakistan inaingia upande wa Kaskazini.
Iran ndiyo ambayo imechukua eneo kubwa la mlango bahari wa Hormuz. Zama za Iran ya kale, Hormuz ilikuwa bandari ya kimkakati ya nchi hiyo ya Kiajemi. Upande wa pili, Yemen ndiyo yenye eneo kubwa kwenye Mlango Bahari wa Bab el Mandeb.
Sasa Mlango Bahari wa Bab el Mandeb ukifungwa, wakati huohuo ikiwa kufungwa kwa Hormuz, tayari dunia inasulubiwa, dhahiri mateso ya maisha yanakwenda kuwa makubwa. Inatakiwa jitihada kubwa za kudhibiti ubabe, na kuruhusu mazungumzo yapate ushindi.