Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka viongozi wa timu za mpira wa kikapu ngazi ya mikoa watakaoshindwa kuzipeleka timu zao kushiriki mashindano ya Taifa Cup kwa kisingizio cha kukosa nauli kuachia nafasi zao za uongozi.

Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya timu kutoka mikoa mbalimbali kushindwa kushiriki mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) jijini Dodoma, zikidai kukosa fedha za usafiri.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Makonda alisema viongozi wanaoshindwa kuhakikisha timu zao zinashiriki wanawakosesha vijana wenye vipaji fursa ya kuonyesha uwezo wao, hivyo hawastahili kuendelea kuwa viongozi.

“Mtu yeyote ambaye hatashiriki mashindano haya hadi mwisho, ajiondoe kwenye nafasi yake ya uongozi. Huwezi kuwa kiongozi wa michezo huku ukizima ndoto za vijana wenye vipaji,” alisema Makonda.

Alalamikia viwanja duni

Makonda pia alieleza kutoridhishwa na hali ya miundombinu ya mchezo wa mpira wa kikapu nchini, akisema viwanja vingi havina hadhi ya kuendeleza mchezo huo.

“Ni ukweli usiopingika viwanja vyetu vya basketball havina hadhi, na baadhi ya miundombinu imebadilishiwa matumizi na kuwa maghala ya kuhifadhia vifaa. Hii ni aibu,” alisema.

Aliahidi Serikali kushirikiana na wadau kuboresha miundombinu hiyo ili kuendana na maendeleo ya mchezo.

Awataka wachezaji wa nje warejee

Waziri huyo pia aliwataka wachezaji wa mpira wa kikapu wa Tanzania wanaocheza nje ya nchi kurejea nyumbani ili kusaidia kuijenga timu ya taifa yenye ushindani kwa upande wa wanaume na wanawake.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kukuza michezo kwa lengo la kuibua vipaji, kuimarisha umoja wa Watanzania na kuifanya sekta ya michezo kuwa chanzo cha ajira na ukuaji wa uchumi.

Taifa Cup si kutafuta mabingwa pekee

Makonda aliwakumbusha washiriki kuwa lengo la Taifa Cup si kupata mabingwa pekee, bali pia kuchochea shughuli za kiuchumi na kukuza vipaji vya vijana.

Mashindano hayo yanashirikisha zaidi ya timu 16 za wanawake na takribani timu 24 za wanaume kutoka mikoa mbalimbali nchini.

“Dhamira ya Serikali ni kuona michezo inakuwa sekta yenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa kupitia ajira, ongezeko la kipato na kuzalisha wanamichezo wenye uwezo wa kushindana katika viwango vya kimataifa,” alisema.

Thabeet aridhishwa na mwitikio

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Hasheem Thabeet, alisema ameridhishwa na mwitikio wa timu zilizoshiriki mashindano hayo.

Alisema ushiriki huo unaonyesha dhamira ya kweli ya kukuza mchezo wa mpira wa kikapu nchini, huku akibainisha kuwa Taifa Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana na kuimarisha umoja wa Watanzania kupitia michezo.

Thabeet pia aliwapongeza waandaaji, viongozi wa mikoa, wadhamini na wachezaji kwa ushirikiano wao, akisisitiza kuwa juhudi hizo zitasaidia kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye ushindani mkubwa katika mchezo wa mpira wa kikapu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *