Dar es Salaam. Mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini yamepata msukumo mpya baada ya washiriki wa kampeni ya GGM HIV Kili Challenge kuanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro na kuuzunguka kwa baiskeli, kwa lengo la kuchangisha fedha, kuhamasisha upimaji wa VVU na kupunguza unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na maambukizi hayo.

Washiriki hao waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Julai 22, 2026, tayari kwa safari rasmi itakayoanza kesho, Ijumaa, Julai 24, 2026, ambapo watu 38 watapanda mlima huo kwa miguu, huku wengine 10 wakifanya safari ya kuuzunguka kwa baiskeli kwa muda wa siku saba.

Kampeni hiyo, inayoratibiwa na Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) na wadau wengine, inalenga kuhamasisha jamii, taasisi na kampuni mbalimbali kuchangia rasilimali zitakazosaidia utekelezaji wa afua za kupambana na VVU na Ukimwi.

Akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya GGML, Gilbert Mworia amesema mwitikio wa wadau umeongezeka mwaka huu, jambo linaloonesha dhamira ya pamoja ya kuunga mkono jitihada za kufikia malengo ya kimataifa ya Sifuri Tatu ifikapo mwaka 2030, yanayolenga kutokomeza maambukizi mapya ya VVU, kumaliza vifo vinavyotokana na Ukimwi na kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU.

Tofauti na miaka iliyopita, kampeni ya mwaka huu itaambatana na utoaji wa huduma za upimaji wa VVU na uchangiaji wa damu salama katika maeneo mbalimbali ya wananchi, hatua inayokusudia kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza mwamko wa kujitambua afya zao.

Amesema ongezeko la washiriki na wadau linaonesha jamii inaendelea kutambua umuhimu wa kushiriki katika mapambano dhidi ya VVU. Amesema: “Tunataka kampeni hii iwe chachu ya watu wengi kujitokeza kupima, kupata elimu na kuondoa unyanyapaa.”

Kwa upande wa washiriki, wameeleza kuwa kupanda mlima huo ni zaidi ya changamoto ya kimwili, bali ni ujumbe wa mshikamano na matumaini kwa watu wanaoishi na VVU.

Mmoja wa washiriki aliyewahi kushiriki mara mbili zilizopita, Chitegetse Rushatsi, amesema anajivunia kuwa sehemu ya kampeni hiyo kwa mara nyingine na anaamini atafanikiwa kufika kileleni.

“Tumepokelewa kwa furaha kubwa na tuna matumaini makubwa ya kufika kileleni. Hii ni mara yangu ya tatu kushiriki, na mara zote nimefanikiwa kufika kileleni. Najivunia kuwa sehemu ya historia hii,” amesema.

Kwa mara ya kwanza kushiriki, Martha Daniel amesema awali alikuwa na hofu, lakini alibadilisha mtazamo baada ya kufahamu lengo la kampeni hiyo.

Amesema mbali na kuchangia mapambano dhidi ya VVU, kampeni hiyo pia inaitangaza Tanzania kupitia mlima Kilimanjaro na kuhamasisha utalii wa ndani.

“Ningependa kuona wanawake wengi zaidi wakijiunga na kampeni kama hizi, kwa sababu zinagusa maisha ya watu wengi na zinaonesha kuwa kila mmoja ana nafasi ya kuleta mabadiliko katika jamii,” amesema.

Miongoni mwa washiriki ni Marietha Elius (13), mwanafunzi wa darasa la saba, ambaye anafurahia kupata nafasi ya kushiriki katika kampeni inayobeba ujumbe wa matumaini kwa watu wanaoishi na VVU.

“Ninafurahi kushiriki kuwasaidia wanaohitaji msaada na wakati huohuo kupata nafasi ya kupanda mlima Kilimanjaro, ambao nimekuwa nikiujifunza darasani,” amesema.

Waandaaji wamesema mbali na kuchangisha fedha, kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa kuhusu VVU, kuhimiza wananchi kujitokeza kupima afya zao, kupunguza unyanyapaa na kusaidia utekelezaji wa huduma na miundombinu inayowanufaisha watu wanaoishi na VVU nchini.

Kupitia ujumbe wa “kupanda kwa ajili ya maisha”, washiriki wanatarajia safari hiyo iwe ishara kwamba mapambano dhidi ya VVU yanahitaji ushirikiano wa sekta binafsi, Serikali na wananchi ili kufikia Tanzania isiyo na maambukizi mapya, vifo vinavyotokana na Ukimwi wala ubaguzi dhidi ya wanaoishi na VVU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *