
Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Bukoba imetupilia mbali rufaa ya Abdul Suleiman ya kupinga kifungo cha maisha jela, baada ya kuridhika kuwa ushahidi uliotolewa na watoto wanne waliodai kubakwa na kulawitiwa naye ulikuwa wa kuaminika na uliuthibitisha bila kuacha shaka yoyote upande wa mashtaka.
Katika hukumu iliyotolewa Julai 3, 2026, Jaji Lilian Itemba amesema baada ya kupitia kwa kina mwenendo wa kesi, ushahidi wa mashahidi, vielelezo na hoja za pande zote mbili, Mahakama imebaini kuwa hakuna sababu ya kuingilia hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Bukoba iliyomhukumu Abdul kifungo cha maisha jela.
Mahakama hiyo ilimhukumu Abdul baada ya kumtia hatiani kwa makosa sita, yakiwamo manne ya ubakaji na mawili ya ulawiti dhidi ya watoto wanne wa kike wenye umri wa kati ya miaka saba na tisa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, makosa hayo yalitendeka katika nyakati tofauti kati ya Aprili na Julai 2024, katika eneo la Kashai, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.
Kwa kuzingatia sheria zinazolinda utambulisho wa watoto, waathirika walitajwa kwa herufi za mwanzo za majina yao na umri wao kuwa S.A (9), L.J (7), G.P (7) na G.G (9).
Abdul alishtakiwa kwa kuwabaka watoto wote wanne na kuwalawiti wawili kati yao, ambao ni S.A na G.G.
Ushahidi wa mashtaka
Mahakama imeeleza kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulionyesha watoto hao waliishi katika eneo moja na Abdul na walimfahamu kwa jina la Mzee Abdul. Katika usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi 11 pamoja na vielelezo vitano.
Katika ushahidi wake, S.A alidai Abdul alimshawishi kwa kumpa fedha kabla ya kumbaka na kumlawiti mara kadhaa alipokuwa akitoka shuleni, na alikuwa akimfanyia vitendo hivyo kwenye moja ya mapagala lililojirani na nyumba yake.
L.J. naye alidai kuwa alibakwa mara moja ndani ya choo cha shule baada ya kupewa Sh200 za kununua pipi. Hata hivyo, alisema alikuwa anashindwa kupiga kelele kwa sababu alikuwa anatishiwa na Abdul.
Kwa upande wake, G.P. alieleza kuwa siku ya tukio alikuwa akitoka shule akiwa na S.A. Alidai Abdul aliwabaka wote wawili ndani ya jengo ambalo halijakamilika, huku akisema yeye alikuwa wa kwanza kufanyiwa kitendo hicho na baadaye akamsubiri mwenzake ambaye pia alibakwa.
Naye G.G. alidai Abdul alimfanyia vitendo vya ubakaji na ulawiti mara mbili tofauti. Alieleza kuwa katika tukio la pili alimkuta akiwa amebeba karai la samaki, alimwita na kumpeleka kwenye nyumba ambayo haijakamilika na kumfanyia vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa ushahidi wake, baada ya tukio hilo, Abdul alimweleza kuwa angefika nyumbani kwao akijifanya anauza samaki, kisha ajifanye amepoteza fedha zake na baadaye ampe fedha ili asimweleze mtu yeyote kuhusu yaliyotokea.
Mbali na ushahidi wa watoto hao, Mahakama ilipokea ushahidi wa kitabibu uliounga mkono madai ya kufanyika kwa vitendo hivyo. Wazazi na walezi wa watoto hao pia walitoa ushahidi kuhusu umri wa watoto pamoja na namna walivyobaini matukio hayo, ikiwamo mabadiliko ya kitabia na dalili zisizo za kawaida walizoziona kwa watoto.
Hoja za rufaa
Akiwa hajaridhishwa na hukumu hiyo, Abdul aliamua kukata rufaa katika Mahakama Kuu akitoa sababu tano.
Miongoni mwa sababu hizo alidai Mahakama ya Wilaya ilishindwa kuchambua ipasavyo utetezi wake, kulikuwa na utata katika ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na kwamba makosa aliyoshtakiwa nayo hayakuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Pia, alipinga ushahidi wa utambulisho akidai watoto hao hawakumtambua kwa uhakika.
Upande wa Jamhuri uliipinga rufaa hiyo ukisisitiza kuwa ushahidi uliotolewa na watoto hao ulikuwa wa kuaminika, ulioana na uliungwa mkono na ushahidi wa kitabibu pamoja na ushahidi wa mashahidi wengine.
Mahakama ilivyochambua ushahidi
Akitoa uamuzi wa Mahakama, Jaji Itemba alisema ushahidi wa watoto hao ulikuwa wa kuaminika kwa kuwa kila mmoja alimweleza Abdul kwa sifa zinazofanana, ikiwamo kuvaa kibarakashi, mabuti na kuwa na mapengo.
Amesema kila mtoto alieleza kwa namna yake mazingira aliyokutana na Abdul na jinsi matukio hayo yalivyotokea, hali iliyoonyesha ushahidi wao haukubuniwa wala kupangwa.
“Kila mtoto alitoa simulizi yake binafsi kuhusu tukio lililompata, jambo lililoifanya Mahakama kuridhika kuwa ushahidi wao ulikuwa wa kuaminika,” amesema Jaji Itemba.
Kuhusu hoja ya kutotajwa kwa tarehe kamili za matukio, Mahakama ilisema hilo halikuathiri kesi ya upande wa mashtaka kwa kuwa waathirika walikuwa watoto wadogo wenye umri wa miaka saba hadi tisa ambao hawawezi kutarajiwa kukumbuka kwa usahihi tarehe za matukio yaliyowapata.
Mahakama pia ilikataa hoja ya kuwepo kwa utata katika ushahidi wa mashahidi, ikisema tofauti ndogo zilizojitokeza kuhusu maeneo au mazingira ya matukio hazikugusa kiini cha kesi.
Jaji amesema ushahidi ulionyesha matukio hayo yalitokea katika maeneo tofauti, yakiwamo choo cha shule, jengo ambalo halijakamilika na nyumba ambayo haijakamilika, hivyo tofauti hizo hazikupunguza uzito wa ushahidi uliotolewa.
Aidha, Mahakama ilikubaliana na maelezo ya upande wa mashtaka kuwa watoto hao walichelewa kutoa taarifa kutokana na vitisho walivyopewa na Abdul baada ya kutendewa vitendo hivyo.
Baada ya kupitia hoja zote tano za rufaa, Mahakama ilihitimisha kuwa hakuna hata moja iliyokuwa na uzito wa kubatilisha hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Bukoba.
Kutokana na sababu hizo, Mahakama ilitupilia mbali rufaa ya Abdul Suleiman na kuacha hukumu ya kifungo cha maisha jela iendelee kutekelezwa.