Zanzibar. Wakazi wa Zanzibar sasa watanufaika na mfumo wa kisasa wa usafiri wa umma usiotumia fedha taslim kufuatia uzinduzi rasmi wa mradi wa mabasi yanayotumia umeme (ZanBus), ambapo kampuni ya huduma za kifedha kidijitali Mixx imepewa jukumu la kusimamia mfumo wa malipo kidijitali kupitia kadi janja (Smart Card).

Mradi huo umezinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, ambaye alisema uzinduzi wa ZanBus ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kujenga mfumo wa usafiri wa umma wa kisasa, salama na rafiki kwa mazingira.

Uzinduzi wa mradi huu wa mabasi ya umeme ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yetu ya kujenga mfumo wa usafiri wa umma wa kisasa, salama na rafiki kwa mazingira. Tuliahidi kuanza kutumia usafiri wa umma unaotumia umeme ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuwapatia wananchi huduma bora zaidi. Hii ni hatua ya kwanza, lakini dhamira yetu ni kuendelea kupanua huduma hii hadi kufikia mabasi 500, sambamba na mpango wa Serikali wa kubadilisha magari ya umma kutumia nishati ya umeme. Lengo letu ni kufikia mfumo wa usafiri wenye uzalishaji sifuri wa hewa chafu (zero emissions), kulinda mazingira na kuifanya Zanzibar kuwa mji wa kisasa unaotoa huduma bora kwa wananchi wake, alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyi.

Akizungumza kama mwekezaji mkuu wa mradi huo, Mkurugenzi Muendeshaji wa ZSSF, Nassor Shaaban Ameir, alisema mradi wa ZanBus ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuleta manufaa ya muda mrefu kwa wananchi na uchumi wa Zanzibar.

Mradi wa ZanBus ni uwekezaji wenye manufaa ya muda mrefu kwa wananchi wa Zanzibar. Mbali na kuboresha huduma za usafiri wa umma, utaongeza matumizi ya teknolojia, utalinda mazingira na kuchochea ukuaji wa uchumi. Kama ZSSF, tunajivunia kuwa sehemu ya uwekezaji huu unaolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya Zanzibar,” alisema Ameir.

Kupitia mfumo huo, abiria hawatalazimika tena kubeba fedha taslim wanaposafiri. Badala yake, watatumia kadi janja inayowezeshwa na mfumo wa Mixx kulipia safari zao kwa haraka, usalama na urahisi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi  Uendeshaji wa Mixx, Arnold Ngarashi, alisema ushirikiano huo ni hatua nyingine muhimu katika kuifanya Zanzibar kuwa kinara wa matumizi ya huduma za kidijitali nchini.

Katika zama hizi za uchumi wa kidijitali, usafiri wa kisasa haukamiliki bila mfumo wa malipo ya kisasa. Kupitia Mixx, wananchi wataweza kuongeza salio la kadi zao kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi au mtandao wetu wa mawakala takribani 20,000 uliopo kila kona ya Zanzibar. Lengo letu ni kuhakikisha huduma ya ZanBus inakuwa rahisi, salama na inamfikia kila mwananchi, alisema Ngarashi.

Alisema mfumo huo utaongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato, kuboresha uzoefu wa abiria na kuweka msingi wa kuunganisha huduma nyingine za kidijitali katika sekta ya usafiri siku zijazo.

Ngarashi amesema ushiriki wa Mixx katika mradi wa ZanBus unaendelea kuonyesha dhamira ya kampuni hiyo ya kuwekeza katika suluhisho za malipo zinazorahisisha maisha ya wananchi na kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo usafiri, biashara na huduma za umma.

Alibainisha kuwa pamoja na huduma za Mixx, kampuni dada za Yas na Yas Fiber zinaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali, ikiwemo uwekezaji wa takribani Sh300 bilioni unaofanywa na Yas Fiber kupanua mtandao wa mkonga wa mawasiliano visiwani humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *