Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps, amesema alikuwa na mpango wa kumbadilisha Kylian Mbappé mapema kabla ya kupata maumivu ya kifundo cha mguu yaliyopelekea kurejea Real Madrid kwa ajili ya kuanza matibabu. 

Maumivu hayo yanamfanya mshambuliaji huyo kukosa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Iceland itakayochezwa leo Jumatatu Oktoba 13, 2025 kwenye Uwanja wa Laugardalsvöllur mjini Reykjavík.

Mbappé alipata majeraha kwenye kifundo cha mguu wa kulia wakati wa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Azerbaijan, Oktoba 10, 2025, ambapo Ufaransa iliibuka na ushindi wa 3-0 jijini Paris.

MBAP 01

Kufuatia hatua hiyo, Deschamps amekanusha madai kuwa hakumlinda vya kutosha nyota huyo wa Real Madrid, ambaye alifunga bao lake la 53 kwenye mechi za kimataifa, na kumfanya azidi kuikaribia rekodi ya mabao ya Olivier Giroud.

“Je, alipaswa kucheza muda wote huo? Tunaweza kujiuliza hilo,” Deschamps amekiambia kituo cha Telefoot cha Ufaransa.

“Nilizungumza sana na Kylian, kabla ya mechi, wakati wa mapumziko, na hata kipindi cha pili.

“Maumivu hayakuwa mabaya sana. Hakuhisi maumivu makali zaidi, lakini aligongana na wachezaji wa timu pinzani mara kadhaa. Kabla sijambadilisha, alipigwa tena sehemu ileile yenye maumivu.”

Deschamps pia amethibitisha kuwa kipa wa AC Milan, Mike Maignan, atavaa kitambaa cha unahodha katika mechi dhidi ya Iceland, akichukua nafasi ya Mbappé.

MBAP 02

Wakati huohuo, Benjamin Pavard amechukua nafasi ya Ibrahima Konaté, beki wa kati aliyerejeshwa Liverpool ili kuendelea na matibabu ya jeraha la paja alilolipata kwenye mechi dhidi ya Chelsea. 

Endapo Ukraine itashindwa kuifunga Azerbaijan mjini Krakow leo na Ufaransa ikaifunga Iceland, itafuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2026 katika nchini za Marekani, Mexico na Canada.

Hadi sasa Ufaransa inaongoza msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi 9, ikifuatiwa na Ukraine yenye pointi 4 na Iceland inashika nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 3, huku Azerbaijan ikiburuza mkia kwa kuwa na pointi 1.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *