
Makubaliano ya usitishwaji mapigano katika Ukanda wa Gaza yametishiwa siku ya Jumapili, Oktoba 19, baada ya jeshi la Israel kusema kuwa limefanya mashambulizi ya anga katika eneo la kusini mwa Palestina kujibu mashambulizi ya Hamas dhidi ya ngome zake, madai ambayo yamekanushwa na Hamas.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Je, usitishaji vita huko Gaza utadumu kwa muda mrefu zaidi? Jeshi la Israel limetangaza kuwa limeanzisha mashambulizi mapya siku ya Jumapili alasiri katika eneo la kusini mwa Palestina “dhidi ya malengo ya magaidi wa Hamas” “kujibu ukiukaji wa wazi wa usitishaji mapigano.” Hapo awali, wanajeshi wa Israel walifanya mashambulizi na kurusha mizinga huko Rafah (kusini) na Beit Lahia (katikati) kujibu mashambulizi ya Hamas, afisa wa kijeshi wa Israel amesema.
Huko Rafah, “Hamas iliwafyatulia risasi wanajeshi wetu waliowekwa nyuma ya mstari wa manjano” – mstari wa kujiondoa wa jeshi la Israel ulioainishwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalianza kutumika tangu Oktoba 10 – kulingana na afisa huyu. Huko Beit Lahia, wapiganaji wa Kipalestina “waliangamizwa katika shambulio kamili” baada ya kuvuka mstari wa manjano na kuingia katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi. Kwa jumla, jeshi limeripoti kuwa “limeshambulia maeneo kadhaa ya kigaidi,” “ikiwa ni pamoja na hifadhi ya silaha na miundombinu ya chini ya ardhi.” Pia limeripoti vifo vya askari wake wawili katika eneo hilo.
Watu 33 wamefariki
Shirika la Ulinzi la Raia la Gaza limetangaza kwamba mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya takriban watu 33. Ripoti ya awali ilisema idadi ya waliouawa ni takriban 11. Miongoni mwa wahasiriwa ni watu sita waliouawa katika shambulio la Israel huko Al-Zawaida, katikati mwa eneo hilo, kwenye “kundi la raia,” wote waliohamishwa kutoka maeneo ya kaskazini, amesema Mahmoud Bassal, msemaji wa Shirika la Ulinzi wa Raia.
Shambulio lingine, dhidi ya “mahema ya watu waliokimbia makazi yao karibu na Khan Younis (kusini), pia limeua mwanamke na watoto wawili,” ameongeza. Pia amehesabu watu wengine wawili waliouawa huko Al-Zawaida, wawili huko Nusseirat (katikati), na wawili huko Jabalia (kaskazini). Shirika la Ulinzi wa Raia limeripoti vifo vingine sita, wakiwemo watoto, katika masambulizi mawili ya Israel majira ya mchana. Jeshi la Israel limeliambia shirika la habari la AFP kuwa linathibitisha madai haya.
Hamas, kwa upande wake, imehakikisha kwamba haifahamu mapigano yoyote katika eneo la kusini mwa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kwamba maeneo hayo yamesalia “chini ya udhibiti” wa Israel. Hamas ambayo kimethibitisha tena wakati huo huo “dhamira yake kamili ya kutekeleza kila kitu ambacho kimekubaliwa,” imeshutumu Israel kwa “kubuni visingizio” vya kuanzisha tena mashambulizi yake huko Gaza.
Kuibuka tena kwa ghasia hizo kunafuatia matamshi ya Benjamin Netanyahu siku ya Jumamosi, ambaye alibainisa juu ya kupokonywa silaha kwa Hamas kama sharti la kumaliza vita, huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kuhusu suala la kubadilishana miili kati ya Israel na Hamas.
Hali inaweza kuwa ngumu zaidi, kwani Marekani inadai kuwa na “taarifa za kuaminika” kuhusu shambulio linalokaribia la Hamas dhidi ya raia wa Palestina huko Gaza, anaripoti mwandishi wetu huko Jerusalem, Michel Paul. Shambulio hili lililopangwa, ikiwa litathibitishwa, litakuwa ukiukaji wa makubaliano na kuhatarisha maendeleo ya hivi karibuni. Katika kujibu, Hamas imesema kwamba “hali inayojiri kwa sasa inaonyesha kinyume,” na imeshutumu vikosi vya Israel kwa “kuunda magenge ya wahalifu wenye silaha” watakaohusika na mauaji na uporaji wa misaada ya kibinadamu. Hamas inahalalisha hatua yake ya polisi kama “wajibu wa kitaifa.”
Mvutano mpya katika Ukingo wa Magharibi
Hali pia ni ya wasiwasi katika Ukingo wa Magharibi, ambapo mwandishi wetu wa Ramallah, Lucas Lazo, anaripoti uingiliaji kati wa kikosi maalum cha Israel mapema Jumapili asubuhi katika kambi ya wakimbizi ya Al Ain, magharibi mwa Nablus. Wakaazi walisikia milio ya risasi na kusababisha kupigwa risasi kwa mtu mwenye umri wa miaka 42, ambaye alifariki kutokana na majeraha yake. Mapema usiku, jeshi la Israel lilifanya operesheni kubwa katika mji wa Tubas, na kupeleka vitengo kadhaa vya askari wa nchi kavu vikitanguliwa na tingatinga.
Wapalestina wanne walikamatwa, nyumba kadhaa ziliharibiwa, na miundombinu ya umma iliharibiwa. Utaratibu huu unakumbusha hatua zilizochukuliwa katika Ukingo wa Magharibi baada ya usitishaji mapigano hapo awali huko Gaza. Mwezi Februari mwaka jana, jeshi lilihamisha watu kutoka kambi za Jenin na Tulkarem baada ya mapigano makali, na kusababisha wakimbizi 40,000 wa Kipalestina kulazimika kuyahama makazi yao.