Abeer Etefa, Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa Kanda na msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, leo amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba tangu usitishaji mapigano uanze tarehe 11 Oktoba, shirika hilo limeweza kuingiza zaidi ya tani 6,700 za chakula kiasi kinachotosha kuwalisha karibu watu nusu milioni kwa muda wa wiki mbili.
“Usafirishaji wa kila siku unaendelea na sasa unafikia wastani wa takriban tani 750 kwa siku,” amesema Bi. Etefa. “Hiyo ni hatua kubwa ukilinganisha na kabla ya usitishaji mapigano, lakini bado ni chini ya lengo letu la tani 2,000 kwa siku.”
Malori yaliyobeba chakula yakisubiri kuingia Gaza.
Kufungua vivuko vyote ni muhimu
Msemaji huyo wa WFP ameeleza kuwa iwapo vituo vyote vya kuvukia mipaka havitatumika, kufikia lengo hilo ni “kitu kisichowezekana.”
Kwa sasa, ni vituo vya Kerem Shalom na Kissufim vilivyoko kusini pekee vilivyo wazi, na uharibifu mkubwa sana unazuia ufikiaji kutoka kusini kwenda kaskazini ambako njaa ilitangazwa mwezi Agosti.
“Tunahitaji Erez, tunahitaji Zikkim, tunahitaji vituo hivi vya kuvukia vifunguliwe,” amesisitiza Bi. Etefa.
Kufikia Gaza Kaskazini kwa misafara mikubwa ni kipaumbele, amesema. “Tumesafisha kwa barabara kuelekea kaskazini kwa kiwango kikubwa,” ameongeza, akieleza kuwa wameondoa vifusi katika maeneo ya mpaka ili kuunganisha na Jiji la Gaza ambako hali ni mbaya zaidi.
“Lakini tunahitaji vituo hivyo vifunguliwe ili tuweze kupeleka misafara mikubwa.”
Chakula kinagawiwa kwa Wapalestina waliokata tamaa.
Msaada unahitaji kusambazwa kupitia vituo 145
Shirika hilo la WFP limeanza kurejesha mfumo wake wa usambazaji wa chakula, likilenga kuongeza misaada kupitia vituo 145 vya usambazaji katika Ukanda wa Gaza. Takribani vituo 26 tayari vimeanza kufanya kazi tena.
“Mapokezi yamekuwa makubwa sana,” amesema Bi. Etefa, akielezea jinsi watu wanavyopokea misaada ya chakula.
“Watu wanajitokeza kwa wingi, wakiwa na shukrani kwa ufanisi wa usambazaji wa msaada wa chakula pamoja na njia yenye heshima wanayoweza kusimama foleni na kupata mgao wao haraka”.
Athari ni kubwa hasa kwa “wale walio hatarini zaidi wanawake, kaya zinazoongozwa na wanawake, na wazee,” amesema.
Watu wana matumaini, lakini “wana matumaini ya tahadhari” kuhusu muda ambao hali ya sasa itadumu, amesema Bi. Etefa.
Wale wanaopokea chakula mara nyingi hula sehemu ndogo ya mgao na kuhifadhi iliyobaki kwa dharura, “kwa sababu hawana uhakika ni kwa muda gani usitishaji mapigano utadumu na nini kitatokea baadaye.”
“Ni amani dhaifu,” amesisitiza Bi. Etefa.
Msaada wa kibinadamu unawasili kwenye ghala la UNICEF Deir Al Balah katikati mwaGaza
Bei za chakula Gaza bado ziko juu
Aidha, amesema kuwa bei za chakula Gaza bado ni za juu mno na bidhaa hazipatikani kwa kiwango cha kuweza kumudu.
“Bado kuna tatizo kubwa la upatikanaji. watu wanaweza kuona chakula sokoni, lakini hakiwezi kunua kwa sababu ni ghali mno,” ameonya.
WFP inawawezesha wale walio katika hatari zaidi ya njaa kupitia malipo ya kidijitali, ambayo yamewaruhusu takriban watu 140,000 kununua chakula kwenye masoko ya ndani, lengo likiwa ni kuongeza idadi hiyo mara mbili katika wiki zijazo.
Msemaji huyo wa WFP amerudia wito wa shirika lake wa kuruhusu usambazaji wa bidhaa za kibiashara kuingia Gaza ili kukamilisha misaada.
“Misaada ya kibinadamu pekee haiwezi kuwa suluhisho la kudumu la kukabiliana na utapiamlo mkali na kuhakikisha mfuko kamili wa chakula,” ameeleza.
Amesisitiza kuwa ni utekelezaji kamili wa makubaliano ya kusitisha mapigano pekee utakaoiwezesha WFP kufanya kazi kwa kiwango kinachohitajika kukabili janga hili. “Kudumisha usitishaji mapigano ni muhimu. Ni njia pekee tunayoweza kuokoa maisha na kupunguza njaa kaskazini mwa Gaza”.