Ripoti hiyo, iitwayo Taarifa Fupi ya Ufuatiliaji ya Wanaorejea Sudan, imetolewa leo tarehe 21 mwezi Oktoba 2025, huku ikionesha kuwa kurejea huko kulitokea kati ya mwezi Novemba 2024 na Septemba 2025, huku familia zikisafiri kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kurejea makwao.

“Wimbi hili la kurejea Khartoum ni ishara ya ujasiri wa wananchi, lakini pia ni onyo,” amesema Ugochi Daniels, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM anayesimamia shughuli za uendeshaji, ambaye hivi karibuni amerejea kutoka ziarani, nchini Sudan.” 

“Nilikutana na watu wanaorejea katika jiji lililoharibiwa na vita, ambapo nyumba zimebomoka na huduma za msingi hazifanyi kazi ipasavyo. Uamuzi wao wa kuanza upya ni wa kutia moyo, lakini maisha bado ni magumu sana. Wakati huo huo, magonjwa kama kipindupindu, homa ya Dengue na malaria yanaendelea kusambaa kote nchini, jambo linalohitaji uwekezaji wa haraka katika maji safi, afya na huduma nyingine muhimu ili watu waweze kuanza maisha mapya kwa usalama.”

Kote Sudan, watu wanarejea katika jamii zao licha ya ukosefu wa usalama unaoendelea na upatikanaji mdogo wa huduma za kimsingi.

Kote Sudan, watu wanarejea katika jamii zao licha ya ukosefu wa usalama unaoendelea na upatikanaji mdogo wa huduma za kimsingi.

Takwimu za kurejea kwa raia

Kwa mujibu wa IOM, Khartoum pekee ilikuwa na makazi ya zaidi ya watu milioni 3.77 waliolazimika kuyahama, ikimaanisha kwamba marejeo ya sasa yanawakilisha asilimia 26 tu ya jumla ya wakazi wote waliohama kutoka jimbo hilo.

Inakadiriwa idadi ya watu milioni 2.7 bado wanaweza kurejea, kutegemeana na hali ya usalama na kibinadamu.

Kwa ujumla IOM imeripoti kurejea kwa idadi ya watu milioni 2.6 nchini Sudan. Kati yao, takribani watu milioni 2 wamerejea kutoka maeneo ya ndani ya nchi, huku 523,844 wakitoka nje ya nchi, hasa kutoka Misri, Sudan Kusini na Libya.

Licha ya matumaini yanayochochewa na kurejea kwa raia katika maeneo yenye utulivu kiasi, hali ya kibinadamu bado ni mbaya sana.Wengi wa wanaorejea wanaishi katika nyumba zilizoharibiwa au vituo vya pamoja bila maji safi, huduma za afya, wala ulinzi. Zaidi ya nusu ya waliorejea wako maeneo ya vijijini, na takribani nusu yao ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

Katika maeneo mengine hali bado ni tete

Katika maeneo mengine ya Sudan, hasa Al Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini ambao bado umezingirwa, hali inatajwa kuwa bado ni tete. Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia mji huo tangu kuanza kwa vita, wengi wao wakitafuta hifadhi huko Tawila, eneo lililogeuka kuwa kambi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao.

Wale waliobaki wanakabiliwa na mashambulizi holela, ukatili wa kijinsia na mashambulizi yenye misingi ya kikabila. Utapiamlo umeenea kwa kasi, hasa miongoni mwa watoto, huku baadhi ya watu wakilazimika kula chakula cha mifugo ili kuishi. 

Wito wa IOM

IOM imesisitiza tena wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mapigano, kumaliza mateso na kutafuta suluhu ya kudumu kwa watu wa Sudan. 

“Wananchi wa Sudan wameonesha ujasiri mkubwa na nia ya dhati ya kujenga upya maisha yao punde tu amani itakaporejea,” imesema IOM.

Ripoti ya Taarifa Fupi ya Ufuatiliaji ya Wanaorejea Sudan ni sehemu ya Mfumo wa Ufuatiliaji wa Uhamisho Duniani wa IOM, unaolenga kusaidia kupanga misaada ya kibinadamu kwa kutumia takwimu sahihi na za kisasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *