Ripoti hiyo, ambayo huchapishwa kila baada ya miaka mitano, imezinduliwa leo tarehe 21 mwezi Oktoba 2025, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kimataifa ya Uangalizi wa Misitu (GFOI) uliofanyika huko Indonesia katika kisiwa cha Bali kilichopo kusini- magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Jakarta
Takwimu za hivi karibuni zimeonesha kuwa misitu inafunika hekta bilioni 4.14 – sawa na takribani theluthi moja ya eneo lote la ardhi duniani. Pamoja na kupungua kwa kasi ya ukataji miti, ripoti ya FRA 2025 inaleta habari njema zaidi kuhusu mustakabali wa misitu: zaidi ya nusu ya misitu duniani sasa ipo chini ya mipango ya usimamizi wa muda mrefu, na karibu robo yake iko ndani ya maeneo yaliyolindwa kisheria.
Hata hivyo, ripoti imeonya kuwa mifumo ya ikolojia ya misitu bado inakabiliwa na changamoto kubwa, huku kasi ya sasa ya ukataji miti ikifikia hekta milioni 10.9 kwa mwaka — kiwango ambacho bado ni kikubwa mno.
Misitu ina umuhimu mkubwa kwa usalama wa chakula, maisha ya jamii za eneo husika, pamoja na kutoa malighafi na nishati endelevu. Pia ni makazi ya sehemu kubwa ya viumbe hai duniani, na huchangia kudhibiti mizunguko ya kaboni na maji duniani, sambamba na kupunguza hatari za ukame, jangwa, mmomonyoko wa udongo, maporomoko ya ardhi na mafuriko.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu, akizungumza katika dibaji ya ripoti hiyo, amesema:
“Ripoti za FRA ndizo tathmini kamili na za uwazi zaidi kuhusu rasilimali za misitu duniani, hali yake, usimamizi na matumizi yake. Takwimu zinazotolewa husaidia jamii ya kimataifa kuelewa mwelekeo wa misitu na mabadiliko yake, na pia kusaidia katika kufanya maamuzi, sera na uwekezaji unaohusiana na misitu na huduma za mfumo wa ikolojia.”
Ukungu unakusanyika kwenye msitu wa mvua wa kitropiki nchini Indonesia
Matokeo muhimu ya FRA 2025
l Ueneaji wa misitu:
Misitu inachukua hekta bilioni 4.14, sawa na asilimia 32 ya uso wa dunia, au takribani nusu hekta kwa kila mtu. Karibu nusu ya misitu yote iko katika maeneo ya kitropiki.
l Kupungua kwa upotevu:
Kasi ya upotevu wa misitu duniani imepungua kutoka wastani wa hekta milioni 10.7 kwa mwaka katika miaka ya 1990 hadi hekta milioni 4.12 katika kipindi cha 2015–2025.
l Ukataji miti na upanuzi wa misitu:
Ukataji miti umeshuka hadi hekta milioni 10.9 kwa kipindi cha mwaka (2015–2025), ikilinganishwa na hekta milioni 17.6 katika 1990–2000. Hata hivyo, kasi ya upanuzi wa misitu pia imeshuka kutoka hekta milioni 9.88 (2000–2015) hadi milioni 6.78 (2015–2025).
l Misitu inayojirejesha kiasili:
Inachukua asilimia 92 ya eneo lote la misitu (hekta bilioni 3.83). Ingawa imepungua kwa hekta milioni 324 tangu 1990, kasi ya upotevu imepungua kwa kiasi kikubwa. Upungufu mkubwa zaidi umetokea Afrika na Amerika Kusini, huku Ulaya ikionyesha ongezeko.
l Misitu ya asili ya awali
Inafunika angalau hekta bilioni 1.18 – takriban theluthi moja ya misitu yote iliyoripotiwa. Upotevu unaendelea lakini umepungua kwa nusu ikilinganishwa na mwanzoni mwa miaka ya 2000.
l Misitu iliyopandwa:
Inachukua takribani asilimia 8 ya eneo lote la misitu, sawa na hekta milioni 312. Eneo hili limeongezeka katika kanda zote tangu mwaka 1990, lakini kasi yake imepungua katika muongo wa hivi karibuni.
l Biomasi na kaboni:
Akiba ya miti duniani inakadiriwa kufikia mita za ujazo bilioni 630, huku akiba ya kaboni misituni ikifikia kiwango cha tani bilioni 714.
l Maeneo yaliyolindwa:
Takribani asilimia 20 ya misitu duniani (hekta milioni 813) ipo katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ongezeko la hekta milioni 251 tangu 1990.
l Mipango ya usimamizi:
Zaidi ya nusu ya misitu duniani (hekta bilioni 2.13, au asilimia 55 ya eneo lote) ziko chini ya mipango ya usimamizi, ongezeko la hekta milioni 365 tangu mwaka 1990.
l Magonjwa na majanga:
Moto unaharibu wastani wa hekta milioni 261 kila mwaka, nusu yake ikiwa ni misitu. Mnamo mwaka 2020, wadudu, magonjwa na hali mbaya ya hewa viliharibu hekta milioni 41, hasa katika maeneo ya baridi na ya wastani.
l Umiliki:
Asilimia 71 ya misitu duniani inamilikiwa na serikali, na asilimia 24 ni mali binafsi, na sehemu ndogo iliyosalia ipo chini ya umiliki mchanganyiko au haijulikani.
l Malengo ya usimamizi:
Takribani hekta bilioni 1.2 (asilimia 29 ya misitu) zinatumiwa hasa kwa uzalishaji, na hekta milioni 616 kwa matumizi mengi. Maeneo mengine yametengwa kwa ajili ya uhifadhi wa viumbe hai (hekta milioni 482), ulinzi wa udongo na maji (hekta milioni 386), na huduma za kijamii (hekta milioni 221).
Ripoti imehitimisha kwa kuonesha kuwa, ingawa maendeleo yamepatikana katika kupunguza kasi ya upotevu wa misitu, juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha misitu inasimamiwa kwa uendelevu kwa ajili ya manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.