Ni kauli ya Veronika Profati mnufaika wa mafunzo ya ujasiriamali, uwezeshaji kiuchumi na ukatili wa kijinsia yaliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP hivi karibuni huko Sumbawanga, mkoani Rukwa, kusini-magharibi mwa Tanzania, barani Afrika.

Veronika na wanawake wengine wa vikundi vya uwezeshaji wanawake walishiriki mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoendeshwa na UNDP ambapo Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia, UNDP Clara Maliwa anasema, “tuna program maalumu hapa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuwapatia elimu na ujuzi namna ya kukabiliana na majanga kwanza, lakini pia tunawapatia elimu ya fedha na elimu ya biashara. .”

Mafunzo hayo ni chini ya Mradi wa UNDP wa kukabiliana na majanga katika wilaya ya Sumbawanga. Kata tano ambazo huwa zinakabiliwa zinakabiliwa na majanga mara nyingi ndio zimehusika.

Kwa nini wanawake?

Bi. Maliwa anasema, “tunafanya hivi kwa wanawake hao kwa sababu tunajua wakati wa majanga mwanamke ndiye anayekuwa mhanga wa kwanza ndio mwathirika wa kwanza. Lakini si hivyo tu, mwanamke huyu ndiye wa kwanza katika kuiokoa familia.

Ndio yeye anaangalia watoto ndio yeye ataangalia wale walioathirika zaidi na majanga ndio huyu atahangaika katika kuifikia na kuangalia mazingira ya familia katika wakati ule wa majanga.”

Anaamini kwamba unapomsaidia mwanamke katika masuala haya ya kutafuta fursa au kumpatia elimu ya biashara unamwezesha yeye aweze kujiokoa. Kwanza si yeye peke yake lakini pia na familia yake. “Lakini tunaamini mwanamke akiwa huru kiuchumi, basi familia nzima inaweza ikawa imepata unafuu wa kuweza kupunguza yale madhara kwa sababu mwanamke huyu atakuwa na uwezo wa kununua chakula kingi, hata kuhifadhi ndani, lakini pia anaweza akawa na uwezo wa kuhamisha familia yake pindi anapopata zile taarifa za awali za madhara kulingana na majanga ambayo yanaweza kutokea katika eneo hilo.”

Kwenye mafunzo haya wanawake wengi walikuja na watoto wao wachanga kwa kuwa hawakuwa na mtu wa kuwaachia nyumbani.

Washiriki wa mafunzo ya kukabili ukatili wa kijinsia na madhara ya mabadiliko ya tabianchi yaliyoandaliwa na UNDP Tanzania huko Sumbawanga, mkoani Rukwa, kusini-magharibi mwa Tanzania.

PMO/UNDP Tanzania

Washiriki wa mafunzo ya kukabili ukatili wa kijinsia na madhara ya mabadiliko ya tabianchi yaliyoandaliwa na UNDP Tanzania huko Sumbawanga, mkoani Rukwa, kusini-magharibi mwa Tanzania.

Sasa nitaweza kutumia vema mikopo

Kwa Veronika mafunzo yatamwezesha kujikwamua kiuchumi na kuwa mjasiriamali na kwamba ni bora wamesaidia wanawake kwani majanga yalipokuwamba, “shida kubwa imekuja kwa sisi wakina mama. Baba ana uwezo wa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Mwanamke huwezi kwa sababu una watoto, tumebaki tunaishi maisha ya kuangaika labda uende ziwani ukanunue tu samaki uje uuze. Kilimo kile ambacho tunakipata hamna sasa hivi hata mahindi ukilima unapata kidogo.”

Kwa Asajile Masebu, Mjumbe wa kikundi cha Kitume Nsia  mafunzo yamemwezesha kufahamu kutunza akiba ya fecha kwani awali “Nilipomwaga mbegu za mpunga mafuriko yalikuja yakasomba shamba. Nilikuwa nimetumia shilingi 500,000 za Tanzania kati ya hizo 300,000 mkopo na 200,000 akiba yangu. Sasa nimefahamu unapokuwa katika biashara, usitumie fedha zote weka akiba.”

Kwa mshiriki Mariam Mwambenja mafunzo haya atashirikisha wenzake waliobakia nyumbani. Naye Veronika Kawimbi anasema mafunzo yatamwezesha kufahamu jinsi ya kutumia na kunufaika vema na mikopo.

Mshiriki mwingine Veronika Fungavyema mafunzo yatamwezesha jinsi ya uwekaji kumbukumbu za fedha kwnai, “sijawahi kuingia kwenye vikao vya aina hii kuhusu biashara na miradi.”

Afisa Mtendaji Kata January Masenga akatamatisha kwa kuwasihi wanawake wajitokeza na kuelezea changamoto zinazowakabili ili zipatiwe ufumbuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *