Alipotembelea Birao, mji unao hifadhi wakimbizi wa ndani 16,000 na wakimbizi wa Sudan 27,000, Msuya ameeleza mateso aliyoyaona kwa wakimbizi hao
“Jana nilitumia saa chache na wakimbizi wa Sudan Birao, asilimia 56 kati yao ni wanawake na watoto. Nimeona maumivu, wanawake waliokatwa viungo, lakini walisafiri wakiwa na majeraha yao hadi CAR, kwa sababu ni salama zaidi hapa,” amesema.
Wakimbizi wasimulia hadithi za kusikitisha
Wakimbizi wamemwelezea kuhusu nyumba zao zilizoanguka Sudan na msaada mdogo waliopokea.
“Nchini Sudan nyumba zetu ziliharibiwa. Tulipofika hapa, UNHCR na Serikali walitusaidia na vifaa vya makaazi, lakini si kila mtu alipewa. Kuna familia zenye watoto, wanawake, na wazee bado wanaohitaji msaada,” amesema mmoja wa wakimbizi.
Mwingine akaongeza, “Kabla tulikuwa tunasafiri kufanya biashara na kilimo, lakini sasa hatuwezi kwa sababu ya ukosefu wa usalama. Tunaogopa, hatuwezi kusogea.”
Bi. Joyce Msuya, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN na Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA katika mahojiano na UN News Kiswahili Aprili 2022 New York, Marekani.
Jitihada za wahudumu wa kibinadamu zapongezwa
Licha ya kukatwa kwa ufadhili wa fecha za misaada, Msuya amewapongeza wahudumu wa kibinadamu.
“Nimeguswa sana na kujitolea kwa wahudumu wa kibinadamu hapa, NGOs za ndani, kitaifa, na baadhi ya za kimataifa, wanafanya kazi kubwa kwa jamii, kwa kujiweka hatarini wao wenyewe lakini hawajaziacha jamii,” amesema.
Mahitaji endelevu na maendeleo
Ingawa asilimia 37 ya watu bado wanahitaji msaada, Msuya amebainisha baadhi ya maendeleo “Nilikipokea taarifa Birao kwamba idadi ya watu waliokimbia makwao imepungua. Sehemu ya maendeleo haya miaka miwili iliyopita ni kwa sababu ya usalama na utulivu bora,” amesema.
Msuya amesisitiza umuhimu wa msaada wa kibinadamu sambamba na misaada ya maendeleo.
“Wengi wao walitamani amani, na usalama. Walitamani watoto wao waende shule, akina mama wajawazito waende hospital. Somo kwangu ni kwamba msaada wa kibinadamu lazima ulingane na msaada wa maendeleo, kwa sababu hatuwezi kuzungumza tu huku maisha yakiendelea kupotea,” amesema.
Kwa sasa, mmoja kati ya watu watano raia wa CAR bado yupo akiwa mkimbizi wa ndani au nje ya nchi, huku mamilioni wakihitaji chakula, ulinzi, na huduma za msingi, hasa katika maeneo yaliyo hatarini kutokana na ukosefu wa usalama na mabadiliko ya tabianchi.