Kuanzia kutoa huduma za dharura na kusaidia katika uokoaji, hadi kurekebisha mitambo ya nishati iliyoshambuliwa, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kufanya kazi licha ya upungufu wa rasilimali, mstari wa mbele unaopanuka, na mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya wenzao.

Matumizi makubwa ya ndege zisizo na rubani na mabomu ya kurusha mbali katika vita vya Ukraine yamefanya maeneo makubwa ya nchi hiyo kuwa wazi kwa mashambulizi ya Urusi, jambo linalozidisha ugumu wa kazi ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu  na masuala ya dharura OCHA, ambayo sasa inajiandaa kukabiliana na baridi kali inayojulikana nchini Ukraine.

Andrea De Domenico, Mkuu wa OCHA Ukraine.

© UNOCHA/Yurii Veres

Andrea De Domenico, Mkuu wa OCHA Ukraine.

Anachosema Mkuu wa OCHA Ukraine

UN News imezungumza na Andrea de Domenico, Mkuu wa ofisi ya OCHA nchini Ukraine, kuhusu changamoto anazokabiliana nazo pamoja na timu yake na jinsi wanavyoweza kuendelea kufanya kazi chini ya hatari.

Andrea de Domenico: Rasilimali zetu zinapungua, hivyo tunalazimika kufanya maamuzi magumu. Tumeweka vipaumbele maalum, kama vile kutoa misaada katika maeneo ya mstari wa mbele, kusaidia katika uokoaji, na misaada ya kibinadamu kwa watu waliofurushwa makwao.
Mwaka huu tunalenga zaidi wale wanaoishi karibu na mstari wa mbele wengi wao wakiwa ni wazee walio hatarini na wenye ulemavu wa kutembea ambao wanahitaji msaada.

Zaidi ya hayo, tunapaswa pia kukabiliana na mashambulizi yanayolenga miundombinu ya nishati, jambo ambalo ni changamoto kubwa. Kwa mfano, wiki iliyopita pekee, asilimia 60 ya uzalishaji wa gesi imeharibiwa. Ukiondoa maji na umeme, kuishi katika msimu wa baridi itakuwa kazi ngumu sana.

Kwa msaada kutoka kituo cha Chișinău, Moldova, mzee raia wa Ukraine anajifunza njia mpya za kukabiliana na changamoto za ukosefu wa makazi.

Fedha zinazohitajika msimu wa baridi

UN News: Mnahitaji kiasi gani kusaidia wanaohitaji, na mmefanikiwa kupata kiasi gani?
Kwa ajili ya msimu wa baridi pekee, tumeomba dola milioni 277, na takriban asilimia 50 pekee ndizo zimepatikana. Kwa hiyo bado tuna safari ndefu kufikia lengo letu lote.
Kwa bahati mbaya, tukishindwa kufikia kiwango hicho, itamaanisha watu hawataweza kukaa majumbani mwao wakati wa baridi na italazimika kuwahamisha.

Matokeo ya shambulizi katikati mwa jiji la Kharkiv, Ukraine.

Matokeo ya shambulizi katikati mwa jiji la Kharkiv, Ukraine.

Kushambuliwa msafara wa UN

UN News: Wiki iliyopita msafara wa Umoja wa Mataifa ulivamiwa kwa mabomu. Timu yako inakabiliana vipi na msongo wa kisaikolojia wa kufanya kazi katika mazingira kama haya?
Sehemu kubwa ya misaada ya kibinadamu katika mstari wa mbele inatolewa na mamlaka za mitaa na washirika wa ndani, na tunapaswa kutambua kazi kubwa wanayofanya kila siku.
Wamekuwa wakikumbana na mashambulizi ya aina hii mara kwa mara. Mwaka huu pekee tumeorodhesha zaidi ya matukio 100.

Kumekuwa na mashambulizi ambayo tulipata madhara kwa bahati mbaya, lakini hili ndilo shambulio la kwanza moja kwa moja dhidi ya msafara wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa. Bila shaka, lilikuwa jambo la kushtua.

Baada ya tukio hilo, niliiambia timu kwamba hili ni moja ya hatari tunazopaswa kukabiliana nazo. Wenzetu wa usalama wa Umoja wa Mataifa walifanya kazi vizuri sana nasi na walifanikiwa kulinda maisha ya wale waliokuwa kwenye operesheni hiyo.

Inahitaji uamuzi, ujasiri na motisha kubwa kuendelea kufanya kazi, lakini ndivyo ilivyo kufanya kazi za kibinadamu katika eneo la vita kunahitaji moyo wa kujitolea kusikokatishwa tamaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *