
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa leo Novemba 03 jijini New York, Marekani, Haq amesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za vifaa, baada ya uchafu na barabara zilizoharibiwa kuzuia ufikiaji wa baadhi ya maeneo yaliyoathirika sana. “Tunaendelea kufanya tathmini, na OCHA inaratibu juhudi za usimamizi wa taarifa,” amesema, akiongeza kuwa wanachama zaidi wa Timu ya Umoja wa Mataifa ya Tathmini na Uratibu wa Majanga (UNDAC) wamewasili nchini Jamaica leo ili kuimarisha mwitikio wa moja kwa moja.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kwa ushirikiano na wakazi wa eneo hilo, limeanzisha ghala la muda la kuhifadhia misaada katika eneo la kanisa lililoko mjini Santa Cruz, katika Parokia ya Mtakatifu Elizabeth. Eneo hilo litakuwa kituo kikuu cha kusambazia misaada kuelekea magharibi mwa nchi, ambako kimbunga kimeleta uharibifu mkubwa.
Cuba
Kuhusu Cuba, Haq amesema Umoja wa Mataifa imekamilisha mpango wa dharura wa utekelezaji, ukilenga hasa eneo la mashariki mwa nchi, ambalo limeathiriwa zaidi na kimbunga hicho. “Tutawapa maelezo zaidi kuhusu mpango huo kesho,” aliwaambia waandishi wa habari.
Katika maeneo yaliyoathirika, vituo vya afya 300 na shule 600 vimeripotiwa kuharibiwa vibaya, huku takribani watu 25,000 wakiendelea kukaa katika vituo vya hifadhi. Upatikanaji wa umeme, maji safi, na dawa unabaki kuwa changamoto kubwa.
Kukabiliana na mahitaji ya haraka ya kiafya, shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limetuma vifurushi vya matibabu kwa ajili ya watu 90,000, vikiwemo dawa muhimu, nyavu za mbu, na chumvi za kurejesha maji mwilini ili kuzuia magonjwa ya kuambukizwa na mbu na upungufu wa maji mwilini kwa watoto. Wakati huo huo, WFP inatoa msaada wa chakula kwa watu 180,000 walioathirika.
Mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alizungumza kwa simu na Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holness, akielezea ushirikiano na mshikamano na Serikali na wananchi wa Jamaica. Guterres alisisitiza kuwa “msaada wa kimataifa ni muhimu sana wakati huu,” na akatoa wito wa kuhamasisha rasilimali kubwa kukabiliana na uharibifu ulioachwa na Kimbunga Melissa.
Ili kuimarisha juhudi za misaada, Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF) umetenga dola milioni 4 kusaidia operesheni za dharura, zikiwemo huduma za chakula, afya, maji, makazi, vifaa vya usafirishaji, usafi na unawaji mikono.
Haq amesisitiza tena dhamira ya Umoja wa Mataifa kusaidia nchi zilizoathirika kupitia uratibu wa misaada ya kibinadamu:
“Tunasimama kwa mshikamano na watu wa Jamaica, Cuba na jamii zote zilizoathiriwa na Kimbunga Melissa wakati wanapoanza safari ndefu ya kujenga upya maisha yao,” amesema.