Dar es Salaam. Yanga imeamua kucheza mechi zake za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa uamuzi huo umekuja baada ya tathmini ambayo uongozi wa klabu hiyo umeifanya baada ya kupangwa kwa makundi ya mashindano hayo.

Yanga imepangwa katika kundi B la mashindano hayo ikiwa na timu za Al Ahly (Misri), AS FAR (Morocco) na JS Kabylie (Algeria).

“Ukiangalia hilo kundi ambalo lina timu nne, kundi B ni kundi ambalo kila mmoja ambaye anafahamu mpira, kila mmoja ambaye anafuatilia mpira wa Afrika vizuri na kila mtu ambaye anafuatilia kwa ukaribu ubora wa ngazi ya klabu Afrika, atakiri kwamba kundi hili ni gumu na kwa lugha ya kimpira tunaliita kundi la kifo.

“Sio kundi jepesi na sio kundi lelemama na sisi uongozi wa Young Africans tunakiri kwamba hili ni kundi gumu na ni kundi ambalo halitabiri hadi sasa hivi na yoyote anaweza kuwa na nafasi ya kuelekea kwenye hatua ya robo fainali.

“Na sisi kama klabu tunaanza mipango yetu sasa hivi kuhakikisha tunakuwa timu moja katika mbili ambazo zitafuzu kuelekea hatua ya robo fainali. Tayari ratiba imeshatangazwa kwa maana mechi zitakavyokuwa. Young Africans tutaanzia mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya FAR Rabat, baada ya hapo tutasafiri kwenda Algeria kucheza na JS Kabylie,” amesema Kamwe.

Kamwe amesema kuwa mechi tatu za hatua ya makundi watacheza New Amaan Complex hivyo mashabiki wa soka visiwani Zanzibar wajiandae kuipokea timu hiyo.

“Kuelekea mechi hizi za Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi baada ya kufanyika tathmini ya kina na kuzingatia maslahi mapana ya klabu yetu, nipende kuwatangazia ndugu zangu waandishi wa habari, wanachama na mashabiki wa klabu yetu ya Young Africans, mechi za klabu yetu kwenye hatua ya makundi zitafanyika kwenye visiwa vya Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

“Kwa hiyo mechi zote tatu za nyumbani za klabu yetu zitapigwa Zanzibar kwenye Uwanja wa Nrw Amaan Complex. Baada ya hapo tukifuzu kwenda mbele, kama kuna utaratibu mwingine tutakuja kuwatangazia,” amesema Kamwe.

Uamuzi wa Yanga kwenda New Amaan Complex utafanya Uwanj huo kutumika na klabu tatu katika hatua hiyo ya makundi, nyingine zikiwa ni Azam FC na Singida Black Stars zilizopo katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Awali Yanga ilikuwa inautumia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambao sasa utatumiwa na Simba pekee kwenye hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *