Oktoba 28, 2025, habari iliyopenya Kenya ilikuwa ripoti ya Umoja wa Afrika 2025. Mtandao wa The Star, Kenya, ulichapisha habari kuhusu ripoti ya Uhusiano wa Kikanda Afrika (ARI) kwa mwaka 2025. ARI ni ripoti ambayo hutolewa na Umoja wa Afrika, kuonesha maendeleo ya kanda kiuchumi.

ARI ni ripoti ambayo huandaliwa kwa ushirikiano wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Kamisheni ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika (ECA), Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), vilevile Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs). Ripoti hiyo ilionesha kuwa Tanzania ina mwendo mzuri wa uzalishaji na uongezaji thamani bidhaa dhidi ya uuzaji wa malighafi.

Kwa Afrika Mashariki, Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa mwendo mzuri wa kiuchumi. Burundi inashika nafasi ya pili, ikifuatiwa na Kenya. Nchi za Uganda, Rwanda na Sudan Kusini zipo chini. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Somalia, zipo mkiani. Kwa Tanzania, hiyo ilipaswa kuwa habari njema ya mwendo wa kiuchumi.

Oktoba 29, 2025, ni siku ambayo Watanzania walipiga kura kuchagua viongozi katika muhula mpya wa 2025 – 2030. Ripoti ya AU (ARI), ilipaswa kuwajaza Watanzania matumaini ya mwenendo mzuri wa taifa lao kiuchumi. Asubuhi, siku ya kupiga kura, hali ilikuwa shwari. Utaratibu wa kupiga kura ulikuwa mzuri. Hakukuwa na foleni vituoni.

Jua la mchana likianza kuchukua nafasi, ripoti za ghasia zikaanza kuripotiwa. Ulikuwa mwanzo wa siku tatu ngumu na nzito kwa taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vifo na majeruhi wengi. Mali za umma na watu binafsi, zikaharibiwa na nyingine kuchomwa moto. Agizo la watu kutotoka nje kuanzia saa 12:00 jioni likatolewa.

Huduma za kijamii zikawa shida. Watanzania waliozoea amani na kuishi kwa upendo na utulivu, wakaogopa kutoka nje hata katika muda walioruhusiwa.

Wenye maduka waliogopa kufungua, maana wengi walivamiwa na kuibiwa. Watanzania wengi maisha yao hutegemea kutoka ndiyo wapate riziki.

Wakageuka ombaomba. Anayeombwa naye anaomba. Siku tatu za giza, zikaongeza mbili za dhiki.

Novemba 3, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia hotuba yake ya uapisho, aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha maisha ya Watanzania yanarejea kama kawaida.

Novemba 4, 2025, Watanzania wakawa sawa na waliotoka kifungoni. Walirejea kazini wakiwa na wasiwasi. Hofu ni ghasia kuibuka kwa mara nyingine.

Nikatazama ripoti za vyombo vya habari vya kimataifa, DW na Al Jazeera. Utangulizi wa ripoti zao ni maandamano kwenye nchi ambayo inafanya vizuri kiuchumi.

Hili linapaswa kumshangaza kila mtu. Taifa ambalo linatembea vizuri katika mwendo wa kiuchumi, inawezekana vipi watu kuingia barabarani?

Ripoti za Benki ya Dunia na Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF), zilionesha afya ya kifedha ya Tanzania inazidi kuimarika. Ukuaji wa Pato la Ndani la Taifa (GDP), kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ulivuka makisio ya asilimia 5.5 hadi kuwa asilimia 5.6. Sera za kifedha za Serikali ya Tanzania, zimewezesha mfumuko wa bei kugota asilimia 3.1.

Sarafu ya Tanzania imeimarika. Dola ya Marekani inauzwa kwa Sh2,400 kutoka Sh2,800. Mapato ya ndani yameongezeka. Ripoti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Septemba 2025, ilionesha makusanyo ya mwezi ni Sh3.47 trilioni, kutoka Sh1.8 trilioni, ambazo Rais Samia alikuta serikali inakusanya wakati anaapishwa kwa mara ya kwanza kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Machi 19, 2021.

Wingi wa makusanyo ya serikali huakisi mambo mengi chanya; kukua kwa mzunguko wa kifedha, kuongezeka kwa uwekezaji, kushamiri kwa biashara na ongezeko la biashara mpya, mafanikio ya vyanzo vipya vya mapato, nidhamu ya usimamizi wa kodi na kuziba mianya ya rushwa.

Yote hayo ukiyaweka kwenye kapu moja ni kwamba hutokea kutokana na sera nzuri za serikali kifedha.

Duniani kote, ni vigumu watu kuandamana nyakati ambazo nchi yao inafanya vizuri kiuchumi. Mafanikio ya kiuchumi huakisi hali bora za watu, na upatikanaji wa uhakika wa huduma za kijamii. Imetokea Tanzania, mwezi mmoja kabla ya Oktoba 29, 2025, wananchi walikuwa wakilalamika huduma mbovu za mabasi yaendayo kasi, Dar es Salaam, kwa sababu yalikuwa machache.

Mabasi mapya, mengi na ya kisasa, yaliingizwa na kuanza kazi. Kero iliyokuwa inalalamikiwa ikaondoka.

Oktoba 29, 2025, vijana waliyachoma mabasi moto mabasi hayo mapya ambayo yalikuwa mkombozi wa usafiri wa umma. Tafsiri ya matendo hayo ni tata. Nadharia ya vitendo hivyo ni zaidi ya moja.

Jumuiya za Kimataifa zinaita ghasia za Oktoba 29, 2025 ni maandamano. Wapo watu wanahoji, aina gani ya maandamano yaliyojikita kushambulia mali za umma na za watu binafsi? Maandamano gani hayakuwa na mabango ya kuwasilisha ujumbe wa kile walichokitaka kitokee?

Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kupitia kwa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, vilevile Jeshi la Polisi Tanzania, kupitia kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillus Wambura, wameita matukio ya Oktoba 29, 2025 na yaliyoendelea siku iliyofuata, kwamba yalikuwa uhalifu.

Lawama ni kwa waliochochea watu kuingia vurugu. Udanganyifu wa umma ulikuwa mkubwa. Wapo watu, wakijua kabisa wanasema uongo, waliwachochea vijana kuamini kwamba JWTZ lilikuwa tayari kwa mapinduzi ya kiraia, kwamba wananchi wangetoka barabarani, jeshi lingewaunga mkono.

Zipo video zikiwaonesha vijana wakiimba “jeshi jeshi jeshi” ni kwa sababu waliambiwa na wakaamini kuwa Jeshi la Wananchi, lingekuwa pamoja na waandamanaji.

Kauli kuwa Jeshi lilikuwa kinyume na mamlaka za nchi, maana yake unasema Jeshi liliasi na kumkaidi Amiri Jeshi Mkuu. Vijana wakaamini. Kwa nini vyombo havikutoa ufafanuzi mzuri mapema ili kuwalinda vijana na uongo uliotumika kuwachochea?

Zipo taarifa ambazo zilithibitishwa na Rais Samia kuwa sehemu kubwa ya vijana walioshiriki ghasia za Oktoba 29, 2025, si raia wa Tanzania.

Baadhi ya watu hao, kwa mujibu wa Rais Samia, wameshakamatwa tayari. Hili linagusa vyombo vya ulinzi na usalama. Inakuwaje watu wavuke mipaka na waingie Tanzania, kisha kuratibu ghasia bila kuchukuliwa hatua kabla ya madhara?

Rais Samia kupitia hotuba yake ya uapisho, alionesha njia ya namna ya kuelekea kuijenga nchi katika hali ya umoja na mshikamano.

Aliahidi kutumia R4, Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mabadiliko) na Rebuilding (ujenzi mpya wa nchi).

Januari 26 na 27, 2001, Taifa la Tanzania, lilikumbwa na kadhia kubwa ya machafuko.

Dar es Salaam na Ungunja kwa sehemu ndogo, Pemba madhara yalikuwa makubwa zaidi. Baadaye, hali ya utulivu ilipatikana.

Viongozi walitafuta chumba cha mazungumzo. Mwafaka ulipatikana, nchi ikasonga mbele. Hata Januari 20, 1964, uasi wa Jeshi ulitikisa nchi. Hata hivyo, hali ya amani ilirejea.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dola iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, haijawahi kukwama kusuluhisha matatizo yake.

Kama ilivyotokea Januari 26 na 27, 2001, au Januari 20, 1964, bila shaka hata hili la Oktoba 29, 2025, taifa litavuka, litarejea pamoja, tena likiwa imara kuliko mwanzo.

Jambo la muhimu ni kwamba wakati wa kutafuta mwafaka na utatuzi wa kuiendea kesho yenye umoja na upendo miongoni mwa Watanzania wote, hatupaswi kusahau waliotega vigingi njiani, matokeo yake, kama taifa tukajikwaa.

Mwenyezi Mungu awawarehemu waliopoteza maisha. Mwenyezi Mungu ailinde dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mungu ibariki Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *