
Kocha wa zamani wa Azam FC, Marian Marinica ameteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘Warriors’ kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Katika mkataba huo, jukumu la Marinica ni kuiongoza timu hiyo katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Marinica mwenye umri wa miaka 59 anarithi mikoba ya Michael Nees, ambaye aliondoka mwezi uliopita baada ya Zimbabwe kushindwa kushinda mechi katika mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia la FIFA 2026.
Chama cha Mpira wa Miguu Zimbabwe (ZIFA) kimesema kuwa uamuzi wa kumteua Marinica ambaye ni raia wa Romania, unalenga kurudisha makali ya timu ya taifa ya nchi hiyo.
“Chama cha Soka cha Zimbabwe (ZIFA) kinafuraha kutangaza kumteua Marian (Mario) Marinica kama Kocha Mkuu mpya wa Timu ya Taifa ya Wanaume ya Zimbabwe ‘The Warriors’ kwa mkataba wa mwaka mmoja,” imesema taarifa ya ZIFA.
Marinica anayemiliki Leseni ya Daraja la Juu ya Ukocha ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), ana uzoefu wa zaidi ya miaka 25 wa kufundisha na kiufundi alioupata Afrika, Ulaya, Asia na Amerika Kusini.
Hapo awali aliifundisha Malawi, akiiongoza kutinga hatua ya 16 bora katika AFCON 2021.
Pia amewahi kuwa mkurugenzi wa ufundi, mwalimu wa makocha na mshauri wa utendaji kazi, majukumu ambayo ZIFA inasema yanawiana na msukumo wao wa kuimarisha maendeleo ya wachezaji na miundo ya ufundishaji wa ndani.
Marinica anayoejulikana kwa nidhamu ya ufundi na soka la hali ya juu, atasimamia maandalizi ya mechi zijazo za kirafiki dhidi ya Algeria na Qatar kabla ya kuelekeza nguvu zao kwenye kampeni ya Zimbabwe ya AFCON nchini Morocco.
ZIFA iliongezea kuwa rekodi yake ya kujumuisha vipaji vya wachezaji wenye asili ya Zimbabwe walio nje ya nchi hiyo na kukuza ujuzi wa makocha wa ndani ni sifa zinazoenda sambamba na mkakati wa muda mrefu wa shirikisho hilo.
Zimbabwe imepangwa Kundi B la AFCON 2025 ambapo itamenyana na Misri, Afrika Kusini na Angola.