Wawili hao watakutana ikiwa ni siku chache baada ya Marekani kumuondoa Al-Sharaa kwenye orodha ya magaidi. Ikulu ya Marekani, White house kupitia msemaji wake Karoline Leavitt imesema mapema Jumatatu kuwa ziara ya mtawala wa Syria Ahmad al-Sharaa ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia za Rais Donald Trump za kukutana na mtu yeyote duniani mwenye shauku ya amani.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais wa Syria ndani ya ikulu ya Marekani tangu taifa hilo lilipopata uhuru mwaka 1946 kutoka kwa Ufaransa.
Mkutano wa Rais huyo wa mpito wa Syria na Trump unatazamiwa kufanyika baada ya Marekani kuiondolea vikwazo Syria iliyokuwa imeviweka wakati wa miongo kadhaa ya utawala wa familia ya Assad.
Hivi karibuni Rais Trump alimsifu al-Sharaa kwa kile alichokiita kazi nzuri anayoifanya akisema, “Tutakutana, Na ninafikiri anafanya kazi nzuri sana. Anatoka katika sehemu ngumu, lakini ni kijana shupavu. Tulielewana vyema na kuna maendelo makubwa Syria. Tuliiondolea vikwazo kutokana na ombi la Uturuki na Israel”
Ahmad al-Sharaa ambaye kundi lake la waasi lilimwondoa madarakani mtawala wa muda mrefu Bashar al Assad alikutana kwa mara ya kwanza na Rais wa Marekani Donald Trump alipokuwa ziarani nchini Saudi Arabia.
Ziara yake inafanyika baada ya kiongozi huyo wa Syria kuutembelea Umoja wa Mataifa mwezi Septemba na kulihutubia baraza kuu la umoja huo.
Ushirikiano kupambana na IS kujadiliwa
Mazungumzo ya Trump na al-Sharaa yanatarajiwa kujikita katika suala la Syria kujiunga na muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya wanamgambo wa Kundi linalojiita ‘Dola la Kiislamu’ IS.
Pia, baadhi ya vipaumbele anavyotarajiwa kuviweka mezani Al-Sharaa katika mkutano wake na Trump ni kutaka vikwazo vilivyoiadhibu Syria kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na serikali ya Assad na vikosi vya usalama viondolewe kabisa.
Ingawa baadhi ya vikwazo vimeondolewa kwa sasa na Trump, kuvifuta kabisa kunahitaji bunge lichukue hatua.
Itakumbukwa kuwa kipindi cha nyuma, Marekani iliwahi kutangaza zawadi ya dola milioni kumi za Kimarekani kwa atakayefanikisha kumkamata Ahmed al-Sharaa aliyewahi kuwa na uhusiano na kundi la al-Qaida.