Noluthando katika video hiyo anazungumza akiwa nyuma yake kukiwa na lundo la taka za plastiki, ikiwa ni dhahiri kwamba wanalenga kuepusha uchafuzi utokanao na taka za plastiki.
Anasema, “Jina la kawaida ni ‘wakusanyaji taka’ lakini sisi hatuhisi kwamba sisi ni wakusanyaji taka. Tunahisi kwamba sisi ni “warejeshaji” kwa sababu tunatoa vitu vyenye thamani kwenye taka na kurejesha kwa matumizi. Kwa kweli, warejeshaji ni wanamazingira. Wanasaidia jamii kwa kuhakikisha kwamba vitu vyote vinavyoweza kurejelewa vinakusanywa. Kwa kufanya hivyo, wanasaidia pia kulinda mazingira.”
Msitunyanyapae kazi yetu ni ya thamani
Licha ya kazi hiyo wamekuwa wakinyanyapaliwa jambo ambalo anakanusha akisema, “Watu wanahitaji kubadilisha mtazamo wao kuhusu warejeshaji. Warejeshaji wanakabiliana na changamoto za unyanyapaa kila siku, lakini kwa kweli, wao ndio hufika nyumbani kwako kuchambua taka zako. Hii inamaanisha kwamba kiasi cha taka kinachopaswa kupelekwa dampo kitapungua.”
Noluthando Tutani, mwanachama wa Chama Cha warejeshaji wa Mazingira barani Afrika, tawi la Afrika Kusini.
Benki ya Dunia iliona pengo hilo hivyo kupitia mradi wake wa kupitia mradi wake wa PROBLUE wa kulinda bayonuai ya maeneo ya pwani, mwaka 2022 iliwezesha kusajiliwa kwa Chama cha Warejeshaji wa Mazingira nchini Afrika Kusini na sasa kina wanachama zaidi ya 11,000. Chama hiki kimesaidia kutoa fursa za ajira na kuweka Afrika Kusini katika mazingira mazuri.
Faida ya kusajiliwa kwa warejeshaji wa mazingira
Noluthando anasema, “dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba haki za warejeshaji zinalindwa na mazingira ya kazi yanaboreshwa. Usajili ni hatua muhimu sana kwani huu ni wakati ambapo wanaweza kutambuliwa kwa kazi wanayofanya. Na kadi anayopatiwa ya uanachama ni aina ya kitambulisho na pia ni kama leseni ya kufanya kazi yao.
Kwa muijbu wa Benki ya Dunia, nchini Afrika Kusini zaidi ya tani elfu 40 za taka za plastiki hutupwa kiholela kila mwaka, huku kiwango kikubwa kikiishia baharini, hivyo jukumu la warejeshaji hawa wa mazingira ni dhahiri .
Jambo hilo linathibitishwa na Noluthando akisema, “Kazi ambayo warejeshaji hufanya kila siku — mchakato wa ukusanyaji usio rasmi — imewezesha halmashauri kuokoa zaidi ya dola milioni 54 katika matumizi ya nafasi ya madampo. Hii inamaanisha kwamba watatambuliwa kwa kazi wanayofanya na kulipwa kwa huduma wanayotoa kwa mazingira na jamii.”