Naples, Italia. Kocha wa Napoli, Antonio Conte, yuko kwenye hali ya sintofahamu kubwa baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Bologna jana Jumapili usiku matokeo yaliyomfanya aite mkutano wa dharura na uongozi wa klabu hiyo.

Kichapo hicho kimeiondoa Napoli kileleni mwa Serie A, huku mabao ya Thijs Dallinga na John Lucumi yakitosha kuwapa Bologna ushindi katika kipindi cha pili.

Kwa sasa, mabingwa watetezi wa Italia wamepoteza michezo mitano katika mashindano yote msimu huu, na hawajafunga bao hata moja kwenye mechi tatu mfululizo hali ambayo imezua hofu kubwa kuhusu mustakabali wa Conte.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Italia Matteo Moretto, Conte anatarajiwa kukutana uso kwa uso na viongozi wa Napoli kujadili hatma yake baada ya matamshi mazito aliyotoa baada ya kipigo hicho.

Baada ya filimbi ya mwisho, Conte alionekana mwenye hasira kali na hakusita kuwakosoa wachezaji wake:

“Ukishindwa mechi tano, ina maana kuna jambo haliko sawa,” amesema. “Lazima hatua zichukuliwe, kwa sababu sitaki kuandamana na mtu aliyekufa kama ipo lawama, basi nianzie mimi mwenyewe. Tumepoteza umoja; kila mmoja anafikiria matatizo yake. Huwezi kubadilisha moyo wa mtu kwa upasuaji.”

Conte aliendelea kwa kusema kuwa timu imepoteza mwelekeo na ari ya ushindi iliyokuwa nayo msimu uliopita:

“Kuna tofauti kubwa kati ya kufanya mazoezi tu na kucheza kwenye timu yenye matarajio makubwa. Wachezaji bado wanajifurahisha kwa mafanikio ya msimu uliopita, badala ya kupigania sasa. Hatujui kama bado tuna njaa ya ubingwa.”

Kocha huyo mwenye maneno makali pia alikumbusha kuwa baada ya Napoli kushinda Scudetto yao ya tatu hapo awali, waliishia kumaliza msimu uliofuata wakiwa nafasi ya kumi akisema historia inaonekana kujirudia.

“Mara nyingi tunafikiri kwamba bata mbaya anaweza kuwa kasuku mzuri ghafla. Tulifanya mambo makubwa msimu uliopita, lakini sasa tumelegea. Sina uhakika kama bado kuna shauku ile ile ndani ya wachezaji wangu.”

Haya yanakuja wiki tatu tu baada ya Conte kuikosoa hadharani dirisha la usajili la klabu, akisema uongozi ulifanya makosa makubwa kwa kusajili wachezaji tisa wapya akiwemo Kevin De Bruyne na Rasmus Hojlund.

“Msimu huu tulibadilisha wachezaji wengi sana. Nilishaonya mapema kuwa itakuwa ngumu kwa sababu hatukuwa na usawa. Kuna mambo ambayo hayawezi kubadilishwa ghafla, inahitaji muda,” amesema Conte.

Mchezaji Rasmus Hojlund, aliyepo kwa mkopo kutoka Manchester United, alianza vizuri lakini sasa amefunga bao la mwisho mapema mwezi Oktoba. Katika mechi dhidi ya Bologna hakupiga shuti hata moja lililolenga lango, na alipokea kadi ya njano.

Hata hivyo, licha ya kushindwa kung’aa, Conte alimpa sifa pekee kijana huyo:

“Labda ndiye aliyekuwa bora uwanjani kwetu. Alijituma, alishambulia nafasi, na Lucumi alikuwa na wakati mgumu kumdhibiti. Tulipaswa kumpa msaada zaidi. Kwa maoni yangu, alicheza vizuri,” amesema.

Baada ya matokeo hayo, Napoli sasa imeshuka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Serie A, ikiwa nyuma ya vinara na wakikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa Bologna iliyoko nyuma yao.

Hali ndani ya klabu inaonekana kuwa tete, na huenda siku chache zijazo zikawa za maamuzi makubwa kwa Conte, kocha ambaye sasa anazidi kuliacha jina lake likining’inia kwenye mizani ya Napoli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *