Ujumbe wa IOM mjini Belém ni bayana: wakati makazi na riziki za watu zinapotishiwa, wanastahili nafasi ya kubaki salama, kupona na kupanga maisha yao ya baadaye.

Kila jamii inastahili fursa ya kuzoea na kujenga mustakabali salama zaidi, lakini kwa wengi, athari hasi tayari zimekuwa kubwa mno,” amesema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM anayeshughulikia Operesheni, Bi. Ugochi Daniels, ambaye anaiwakilisha IOM katika kikao cha ngazi ya juu cha Nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).

Na pale inapokuwa haiwezekani kubaki, watu wanapaswa kuwa na uwezo wa kuhama kwa usalama na kwa heshima. Hilo ndilo tunalolenga – kutafuta suluhisho za vitendo zinazolinda maisha na kuimarisha jamii.”

Mamia ya watu wamefariki katika tetemeko la ardhi mashariki mwa Afghanistan. Timu za IOM zimefika kutoa usaidizi muhimu kwa jamii zilizoathirika.

Takwimu

Kwa mujibu wa takwimu za IOM, mwaka 2024 pekee majanga yalichangia kuhama kwa idadi ya watu milioni 45 ndani ya nchi zao, na kusababisha hasara ya zaidi ya kiasi cha dola bilioni 240. Nyuma ya takwimu hizi wapo wakulima waliopoteza nyumba zao kutokana na mafuriko, na watoto ambao shule zao zimebomolewa.

IOM inaendelea kushirikiana na serikali na wadau wa ndani kusaidia jamii kupona, kujenga upya na kujiandaa kwa majanga yajayo.

Mkutano wa COP30, ambao mwaka huu umeandaliwa na Serikali ya Brazil, ni mkutano wa kwanza wa tabianchi kufanyika katika eneo la Amazon, na unasisitiza uongozi wa watu wa asili, jamii za wenyeji, na makundi mengine yanayoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa kuzingatia kuwa mafuriko, ukame, moto wa nyika na joto kali vinaendelea kulazimisha mamilioni ya watu kuhama makazi yao kila mwaka, IOM imesisitiza kwamba maamuzi yatakayofikiwa mjini Belém lazima yalinde haki za watu na kuimarisha uwezo wao wa kuhimili na kuzoea madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Yatarajiwayo

Miongoni mwa matokeo makuu yanayotarajiwa katika COP30 ni kupitishwa kwa Lengo la Kimataifa la Uhimilivu (GGA), ambalo litaweka malengo mahsusi ya kulinda jamii kupitia mifumo ya tahadhari za mapema, kuimarisha riziki na kuboresha makazi salama — hatua muhimu katika kupunguza uhamaji unaosababishwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Malengo haya yanaendana na kazi za IOM, ambapo mwaka 2024 pekee shirika hilo liliwasaidia idadi ya watu zaidi ya 875,000 kupona kutokana na majanga, na kuunga mkono zaidi ya jamii 100,000 zilizokumbwa na majanga, mishtuko ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, kwa lengo la kuwawezesha kujiandaa vyema na changamoto za baadaye.

Aidha, Mpango wa Mpito wa Haki unalenga kuhakikisha kuwa kadri nchi zinavyohamia kwenye nishati safi, wafanyakazi na jamii wanapata ajira zenye staha, ulinzi wa kijamii na njia salama za uhamaji. Wakati huo huo, Mfuko Mpya wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu unakusudia kuelekeza rasilimali kwa jamii zilizo hatarini, ili ziweze kujenga upya maisha yao kwa heshima na uthabiti.

Kwa kuwa maamuzi yatakayofikiwa mjini Belém yataathiri maisha kwa miaka mingi ijayo, ushiriki wa IOM katika mkutano wa COP30 unaongozwa na lengo kuu moja: kuhakikisha kuwa watu walioko mstari wa mbele wa janga la mabadiliko ya tabianchi hawasahauliki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *