Dar es Salaam. Kwa miaka zaidi ya 25, nyimbo za Lady Jaydee zimesikika kila sehemu na kumpatia mashabiki wengi pamoja na umaarufu mkubwa, mambo yanayomfanya sasa kusimama kama chapa yenye heshima kubwa.

Hata hivyo, kuna mambo mengi hutokea nyuma ya pazia kabla ya wimbo wake au aliyoshirikishwa kusikika masikioni mwa shabiki, baadhi ya mambo hayo, ni haya yafuatayo.

1. Wimbo wa Lady Jaydee, I Dont Care (2019), jina hilo alipewa na mtayarishaji wake, Man Walter kutokea studio za Combination Sound, ambaye pia ameandaa ngoma za Jide kama Joto Hasira (2013) na Yahaya (2013).

2. Katika kuandaa wimbo wake, Sawa na Wao (2016), Lady Jaydee alishirikiana na Fancy Fingers, mwimbaji na mpiga gitaa wa kundi la Sauti Sol kutokea Kenya.

3. Hata hivyo, Jide hadi sasa hajawahi kushirikiana na Sauti Sol. Kundi la muziki kutokea Kenya alilofanya nalo kazi ni H_art The Band waliosikika katika wimbo wake ‘Rosella’ kutoka katika albamu, Woman (2017).

4. Wimbo wa Lady Jaydee ‘Boyfriend wa Dar’ ambao ulitoka Novemba 2018, kwa mara ya kwanza ulirekodiwa miaka 22 iliyopita, na ulitakiwa kuwamo katika albamu yake ya pili, Binti (2003) ila ukawekwa kando.

5. Kuna baadhi ya vesi zake katika nyimbo za rap, Jide ameandikiwa na wasanii wanaofanya aina hiyo ya muziki, ila akachana mwenyewe akirejea zama alizokuwa akiichana mistari ya Mc Lyte.

Waliomwandikia ni Professor Jay katika wimbo wao walioshirikiana wa Nimeamini (2006). Pia One The Incredible alimwandikia vesi ya kwanza ya ngoma yake, I Miss You (2017).

6. Licha ya kutoka kimuziki kipindi kimoja, hadi sasa Lady Jaydee na Stara Thomas hawajawahi kufanya kolabo yao!. Au ndio mafahali wawili hawakai zizi moja?

7. Stara alivuma baada ya kuachia albamu, Nyuma Sitorudi (2000) ikiwa na wimbo maarufu, Mimi na Wewe. Huku Lady Jaydee akiibuka na albamu yake, Machozi (2001), wimbo pia uliobeba jina la albamu hiyo.

Na nyimbo zote hizo zilitayarishwa na Master J kutokea MJ Records, zamani MJ Production, studio iliyoanza kazi katikati mwa miaka ya 1990.

8. Katika wimbo wa Lady Jaydee, Machozi (2000), upande wa utayarishaji Master J alishirikiana na Rajab Marijani ambaye alipiga gitaa na kuufanya wimbo huo wa RnB kuvutia zaidi.      

9. Lady Jaydee ameandika mwenyewe vesi aliyoimba katika wimbo wa Matonya, Anita (2007), ambao aliyekuwa mumewe na meneja wake, Gardner G. Habash ndiye alimshawishi Matonya kumshirikisha Jide.

10. Kwa mara ya kwanza Lady Jaydee na Luciano, msanii wa raggae kutokea Jamaica, walikutana nchini Kenya katika kituo kimoja cha runinga, kisha baadaye wakaja na kolabo yao, Anaweza (2018) iliyofanya vizuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *