Denmark. Ukistaajabu ya Musa utayaona ya filauni! Nchini Denmark eneo la Aalborg wadau wa burudani wameanzisha bustani ya muziki ‘Music Park’ au “De Syngende Træer” ambayo kila mti umefungwa spika yenye wimbo wa msanii aliyewahi kutumbuiza eneo hilo, ambapo mti wenye jina la msanii unayemkubali ukibonyeza kitufe cha kijani kilichopo katika spika wimbo wake utaanza kupiga (kusikika).

Inaelezwa kuwa upandaji wa miti na usimikaji spika katika eneo hilo ulianzishwa na Sir Cliff Richard mwaka 1987. Ambapo baada ya kupiga show ya nguvu Aalborg aliamua kuanzisha mradi huo wa kipekee kwa wasanii kuacha kumbukumbu zao kwa njia ya miti.

Baada ya hatua hiyo kupokelewa kwa ukubwa na wakazi wa jiji hilo ndipo wasanii wengine waliamua kuacha kumbukumbu zao. Kila mti uliwakilisha msanii na nyimbo zake maarufu.

Aidha kwa mujibu wa tovuti mbalimbali zinaeleza kuwa lengo la bustani hiyo lilikuwa ni kuhifadhi kumbukumbu za wasanii waliotembelea Aalborg na kutoa burudani ya kipekee kwa jamii. Huku ikiacha historia ya kuwa bustani ya kipekee kuwahi kutokea ambayo si sehemu tuu ya kupata hewa bali kufurahia muziki pia.

Mpaka 2025, takribani miti 94 imepandwa katika eneo hilo, kila mti ukimwakilisha msanii na muziki wake. Ukifika katika eneo hilo moja kwa moja utakwenda kwenye mti wa msanii unayemkubali kisha utabonyeza kitufe cha kijani kwenye spika na baada ya hapo wimbo utaanza kupiga (kusikika).

Baadhi ya wasanii maarufu waliopanda miti pamoja na kuweka spika za nyimbo zao ni Shakira akiweka wimbo wa  “Hips Don’t Lie” na “Waka Waka (This Time for Africa)”, Beyoncé – “Halo”, “Single Ladies (Put a Ring on It)”, Jason Derulo, Prince  “Purple Rain”, “Kiss”, Bob Dylan – “Like a Rolling Stone”, “Blowin’ in the Wind” na wengineo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *