
Paris. Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy ameachiwa gerezani, ikiwa ni wiki tatu tu katika kifungo chake cha miaka mitano baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki katika njama ya uhalifu. Atakuwa chini ya uangalizi wa mahakama huku akiwa haruhusiwi kuondoka Ufaransa kabla kesi yake ya rufaa itakaposikilizwa mwaka ujao.
Oktoba 21, 2025, rais huyo mwenye umri wa miaka 70, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kuhusika katika njama ya kufadhili kampeni yake ya uchaguzi wa 2007 kwa fedha zilizotolewa na rais wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi.
Baadaye, timu yake ya wanasheria iliwasilisha ombi la rufaa ili aachiliwe. Akiandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuachiliwa, Sarkozy amesema: “Nguvu zangu ziko katika lengo moja la kuthibitisha kutokuwa na hatia. Ukweli utashinda… Mwisho wa hadithi bado haujaandikwa.”
Gari la Sarkozy limeonekana likitoka kwenye Gereza la La Santé, mjini Paris, chini ya saa moja na nusu baada ya mahakama kukubali kuachiliwa kwake. Muda mfupi baadaye, alionekana akiwasili nyumbani kwake magharibi mwa Paris.
Christophe Ingrain, mmoja wa mawakili wake, amepongeza kuachiwa mteja wake kama “hatua muhimu” na kusema sasa watajiandaa kwa kesi ya rufaa inayotarajiwa Machi, 2026. Sharti moja la kuachiwa kwake ni kwamba asiwasiliane na mashahidi katika kile kinachojulikana kama “kesi ya Libya” au wafanyakazi wowote wa Wizara ya Haki.
Wakati wa kifungo chake, alitembelewa na Waziri wa Sheria, Gérald Darmanin, tukio lililosababisha mawakili 30 wa Ufaransa kuwasilisha malalamiko dhidi ya Darmanin, wakiashiria mgongano wa kimaslahi kwa sababu Darmanin alikuwa mfanyakazi mwenza wa zamani na rafiki wa Sarkozy.
Akizungumza na mahakama mjini Paris kupitia video Jumatatu asubuhi, Sarkozy alielezea kuwa hajawahi kuwa na wazo la kumwomba Gaddafi fedha.
“Sitakubali kamwe kitu ambacho sijafanya.” Pia alitoa pongezi kwa wafanyakazi wa magereza kwa kuonyesha ubinadamu.
Mke wa Sarkozy, mwimbaji na mwanamitindo, Carla Bruni-Sarkozy, pamoja na watoto wao wawili, walikuwepo katika chumba cha mahakama kumuunga mkono.
Sarkozy ndiye kiongozi wa kwanza wa zamani wa Ufaransa kuhukumiwa jela tangu kiongozi wa wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Philippe Pétain, kufungwa kwa uhaini mwaka 1945.
Tangu aingie gerezani, Sarkozy amekuwa akishikiliwa katika chumba cha peke yake, chenye choo, bafu, dawati, jiko dogo la umeme na TV ndogo – ambazo alilipia €14 (£12) kwa mwezi pamoja na friji ndogo.
Aliruhusiwa kupokea taarifa kutoka nje na kutembelewa na familia, pamoja na mawasiliano ya maandishi na simu, lakini alikuwa katika kifungo cha upweke. Aliruhusiwa kutoka nje ya chumba kwa saa moja tu kwa siku kwa ajili ya mazoezi, ambayo alifanya peke yake.
Walinzi wawili waliwekwa karibu na chumba chake, jambo ambalo Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurent Nuñez alisema lilitokana na hadhi ya Sarkozy.
Sarkozy alikuwa rais wa Ufaranza kuanzia 2007 hadi 2012. Tangu aondoke madarakani, amekuwa akikabiliwa na kesi za uhalifu, na kwa miezi kadhaa ilimbidi kuvaa kifaa cha kielektroniki kwenye kifundo cha mguu baada ya kutiwa hatiani Desemba mwaka jana kwa kujaribu kumuhonga hakimu ili apate taarifa za siri kuhusu kesi nyingine.