
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) amekanusha vikali madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo kaskazini mwa Nigeria.
Mahmoud Ali Youssouf amesema hayo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, ambapo amesisitiza kuwa, hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa mauaji ya kimbari yamefanyika kaskazini mwa Nigeria.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) ameeleza kuwa, mtu anapaswa kufikiria kwa kina kabla ya kutoa matamko ya aina hiyo, akisisitiza kuwa waathiriwa wengi wa mashambulizi ya kundi la Boko Haram ni Waislamu na wala sio Wakristo.
Serikali ya Nigeria nayo pia kwa upande wake, imepinga madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mauaji ya Wakristo nchini Nigeria, ikionya dhidi ya kauli zinazoweza kuchochea mgawanyiko wa kidini au kikabila nchini humo.
Hivi majuzi Trump aliitangaza Nigeria kuwa “Nchi ya Wasiwasi Maalum” siku ya Jumamosi, akionya kuhusu uwezekano wa kuishambulia kijeshi ili “kuwalinda” Wakristo. Alidai kuwa “idadi kubwa” ya Wakristo wanauawa nchini Nigeria.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, imekanusha kama ya uongo na yenye hatari madai kwamba makundi yenye misimamo mikali katika eneo hilo yanawalenga watu wa dini fulani au yanafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo.
Wiki iliyopita, wananchi wa Nigeria walimiminika mitaani katika jiji la Kano, kaskazini mwa Nigeria, kupinga vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani, vya kuivamia nchi hiyo kijeshi.