Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio ametoa wito siku ya Jumatano, Novemba 12, wa kusitishwa kwa kuvipa silaha Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) nchini Sudan, nchi iliyokumbwa na mzozo ambao umezidi kuwa mbaya katika wiki za hivi karibuni.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

“Lazima kitu kifanyike ili kusitisha utoaji wa silaha na uungaji mkono ambao Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinanufaika, wakati vinaendelea kusonga mbele,” Rubio amesema katika mkutano wa kilele wa G7 nchini Canada.

Nchi hii ya tatu kwa ukubwa barani Afrika imekumbwa na mzozo wa madaraka kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vyote vikiwa vinatuhumiwa kwa ukatili, tangu mwezi Aprili 2023. Vita hivyo vimesababisha, kulingana na Umoja wa Mataifa, mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

Akielezea hali hiyo kama “ya kutisha,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kwamba “tatizo la msingi ni kwamba RSF hufanya ahadi na kisha hawaziheshimu kamwe.”

Wiki iliyopita RSF ilidai kuunga mkono pendekezo la kimataifa la makubaliano ya amani ya kibinadamu, lakini wameongeza mashambulizi yao katika eneo kubwa na muhimu la kimkakati la Kordofan.

Alipoulizwa na waandishi wa habari, Marco Rubio alikataa kutaja haswa Falme za Kiarabu, mshirika wa karibu wa Marekani katika Ghuba ambaye mashirika yasiyo ya kiserikali yanaishutumu kwa kuwaunga mkono RSF. Abu Dhabi inakanusha madai.

Silaha zinazotolewa kwa wanajeshi “hupitia baadhi ya nchi; tunajua ni zipi, na tutazungumza nazo ili kuwafanya waelewe kwamba hii itaharibu taswira yao na ya ulimwengu mzima,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

Taarifa ya Marco Rubio ilikuja saa chache baada ya msimamo kama huo kutolewa siku ya Jumatano na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa.

“Ufaransa inaheshimu kwa makini vikwazo vya silaha,” alitangaza Benjamin Haddad, Waziri Mjumbe wa Masuala ya Ulaya, katika Seneti, akiongeza kuwa “ni muhimu sana kwamba nchi zote kuheshimu vikwazo hivi.”

Falme za Kiarabu pia ni mshirika wa karibu wa Ufaransa, hasa katika ulinzi.

Mgogoro nchini Sudan umesababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa na karibu watu milioni 12 kuhama makazi yao. Uliongezeka zaidi baada ya mji wa El-Fasher uliokuwa ukidhibitiwa na jeshi kuanguka mikononi mwa RSF mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu. El-Fasher ilikuwa ngome ya mwisho ya jeshi huko Darfur.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *