Sylvia na Noureddin, walitiwa hatiani kwa ubadhirifu na utakatishaji fedha, kujihusisha na uhalifu na kughushi nyaraka za serikali.
Mahakama hiyo pia ilitoa waranti wa kukamatwa kwa wawili hao.
Pia waliamriwa kulipa mamilioni ya dola kama fidia kwa uhalifu dhidi ya taifa hilo la Gabon.
Mwendesha mkuu wa mashtaka katika Mahakama ya Rufaa ya Libreville Eddy Minang, amesema wawili hao walitawala bila kupingwa na kujaribu kujifanya kama waathirika wa mfumo waliounda.
Minang pia aliwashutumu washtakiwa wote kwa kutumia vibaya hali ya kiafya ya rais Bongo ili kudhibiti fedha za serikali.
Mwendesha mashtaka huyo pia alitoa picha za ndege mbili za kibinafsi zinazodaiwa kununuliwa kwa njia ya utakatishaji fedha na majumba yaliyoorodheshwa ikiwa ni pamoja na jumba la kifahari huko London na Morocco.
Mwishoni mwa wiki Noureddin Bongo alizungumzia kuhusu kutokuwa na imani na mchakato huo wa kisheria akidai kwamba tangu mwanzo kesi dhidi yake na mamaake haikuonesha kuelekea kutowa haki.
” Nadhani mimi na mamangu ni wahanga wa hujuma za kimahakama zilizofanyika. Isitoshe, kesi hii kamwe haijawahi kuwa ya haki kuanzia mwanzo wa mapinduzi ya Oktoba 29 2023, wakati wanajeshi waliovalia kofia za kuficha nyuso walipokuja nyumbani kwangu.”
Wakati wa kesi hiyo, Noureddin, ambaye alishikilia nafasi ya mratibu wa masuala ya urais, alielezwa na mashahidi kama mhusika mkuu aliyetoa amri katika ikulu ya rais baada ya baba yake kupata kiharusi mnamo Oktoba 2018.
Sylvia na Noureddin Bongo walikuwa na ushawishi mkubwa nchini Gabon
Familia hiyo ya Bongo inayoishi London na kushikilia urai wa Ufaransa, ilikataa kushiriki katika kesi hiyo .
Sylvia na Noureddin, walikuwa na ushawishi mkubwa wakati huo wa utawala wa miaka 14 wa Rais wa Bongo.
Ali Bongo alitimuliwa madarakani katika mapinduzi ya mwaka 2023 baada ya kushinda uchaguzi uliokabiliwa na utata ambao jeshi na upinzani zilisema pia ulikumbwa na udanganyifu.
Mapinduzi hayo yalihitimisha miaka 56 ya familia hiyo ya Bongo madarakani.
Babake Ali Bongo, Omar Bongo, alitawala kwa miaka 42.
Kufuatia kutimuliwa kwa Ali Bongo, Valentin na mama yake waliwekwa kizuizini kwa miezi 20 kabla ya kuruhusiwa kusafiri nje ya nchi.