Wafuasi wa Besigye wanasema mateso anayopitia kiongozi wao ni hila za kisiasa za rais Yoweri Museveni na kwa bahati mbaya marais wenzake wa Kenya na Tanzania wamedhihirisha kuungana katika kuwakandamiza wanasiasa wa upinzani kwenye kanda hiyo.

Hivi sasa Mwanasiasa huyo wa upinzani wa siku nyingini nchini Uganda, Kizza Besigye anashikiliwa jela wakati kesi yake ikisubiri kusikilizwa tena Desemba 4 akikabiliwa na tuhuma za Uhaini. Kesi hiyo imekuwa ikipigwa tarehe kila wakati na Besigye akiendelea kuhangaika Jela.

Mwanasiasa huyo alitekwa nyara tarehe 20 Mwezi Novemba mwaka 2024, na  mke wake wakati huo alivifahamisha vyombo vya habari kwamba mumewe alikuwa ametekwa kutoka kwenye hoteli moja ya mjini Nairobi na hakujua aliko.

Wiki moja baadaye, mwanasiasa huyo alifikishwa katika mahakama ya kijeshi Uganda na kusomewa mashtaka ya uhaini na kufanya jaribio la kupindua utawala wa rais Yoweri Museveni ambaye amebaki madarakani takriban miaka 40.

Dkt Besigye bado hajafanikiwa kupewa dhamana

Licha ya mahakama ya kijeshi kufutiliwa mbali baada ya wanasheria kuwasilisha shauri katika mahakama ya juu, Dkt Besigye amendelea kunyimwa dhamana na mahakama mbalimbali za kiraia

Besigye afikishwa mahakama ya kijeshi

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kulingana na wafuasi wake wa chama cha PFF, wamepanga kufanya maombi ya wiki nzima kuanzia leo Jumatatu kuwaombea wafungwa wote wa kisiasa huku wakiwataka wanasheria Afrika Mashariki kuishinikiza mahakama ya Jumuiya hiyo iliyoko Arusha kushughulikia shauri walilowasilisha kukosoa Kenya kwa kuruhusu vyombo vya dola vya Uganda kumteka Dkt Besigye nchini mwao bila kupitia michakato ya kisheria.

Erias Lukwago aidha ameshtumu mienendo ya marais wa Afrika Mashariki kuonekana kushirikiana katika kuwakandamiza wapinzani wao. Amewataja hasa rais wa Kenya, Tazania na pia wa Uganda kutanguliza mashlahi ya kung’ang’ania madarakani badala ya kujenga mazingira ya demokrasia kama wanavyofanya wenzao wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ambayo huchukua hatua pakitokea hali yoyote inayokiuka demokasia na haki za binadamu katika mojawapo ya nchi wanachama wake.

Lukwago amefichua kuwa ni kwa msingi huu ndipo sasa vyama vya upinzani Kenya Tanzania na Uganda pamoja na asasi za kiraia vinazingatia kuunda jukwaa la pamoja kupigania demokrasia na haki za binadamu kanda hii.

Baada ya kikao cha wanahabari, viongozi hao wameelekea gereza kuu la Luzira kwenda kuzindua maombi ya wiki moja wakiwa na Dkt Kizza Besigye. Wiki moja ya maombi ambayo wametangaza inalenga pia wafungwa wote wa kisiasa wakiwemo wale 150 ambao wanaharakati wa Kenya walioachiwa hivi majuzi kutoka kizuizi cha siku 38 Uganda walidai wanaendelea kushikiliwa kule walikokuwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *