Hayo yamebainishwa katika ripoti  mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF iliyotolewa leo, tarehe 20 Novemba 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani.

Ripoti hiyo, Hali ya Watoto Duniani 2025: Kutokomeza Umaskini wa Watoto, Wajibu Wetu wa Pamoja, imechambua takwimu kutoka zaidi ya nchi 130 za kipato cha chini na cha kati, na kupima umaskini wa aina mbalimbali kupitia huduma sita muhimu: elimu, afya, makazi, lishe, maji na usafi wa mazingira.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, watoto milioni 118 wanakosa huduma katika maeneo matatu au zaidi, huku milioni 17 wakikosa huduma katika maeneo manne au zaidi.

Akizungumzia matokeo ya ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell, amesema: Watoto wanaokua katika umaskini bila lishe, makazi salama na huduma za msingi hukumbana na madhara makubwa katika afya na maendeleo yao. Hali hii inaweza kubadilika ikiwa serikali zitawekeza katika sera sahihi.”

Watoto wameketi pamoja katika kituo cha muda ambacho ni rafiki kwa watoto, iliyoko katika eneo la wakimbizi huko Adré, mashariki mwa Chad, wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell.

© UNICEF/Annadjib Ramadane Mahamat

Watoto wameketi pamoja katika kituo cha muda ambacho ni rafiki kwa watoto, iliyoko katika eneo la wakimbizi huko Adré, mashariki mwa Chad, wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell.

Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kusini mwa Asia bado wanabeba mzigo mkubwa

Ripoti imeonesha kuwa viwango vya juu zaidi vya umaskini wa kila aina vinapatikana Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kusini mwa bara la Asia. Mfano, nchini Chad asilimia 64 ya watoto wanakosa takriban huduma mbili muhimu, huku karibu robo wakikosa huduma tatu au zaidi.

Aidha, upungufu mkubwa zaidi ni katika usafi wa mazingira:

  • Asilimia 65 ya watoto katika nchi za kipato cha chini hawana choo salama.
  • Katika nchi za kipato cha kati cha chini, kiwango hicho ni asilimia 26.
  • Katika kipato cha kati cha juu ni asilimia 11.
  • Hali hii inaongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya magonjwa kwa watoto.

Maendeleo yatetereka kutokana na changamoto mpya

Ingawa kiwango cha watoto wanaokosa huduma moja au zaidi kilishuka kutoka asilimia 51 mwaka 2013 hadi asilimia 41 mwaka 2023, ripoti hiyo inaonya kuwa maendeleo hayo sasa yamesimama. Migogoro, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu, madeni ya kitaifa na pengo la teknolojia vinaendelea kuzidisha umaskini.

Wakati huohuo, kupungua kwa misaada rasmi ya maendeleo (ODA) kunatishia ongezeko la watoto wanaokosa huduma muhimu.

Watoto wa shule ya chekechea kwenye mkoa wa Morogoro ulioko mashariki mwa Tanzania wakionesha mbinu za kuhesabia namba zilizotengenezwa na mwalimu wao.

Watoto wa shule ya chekechea kwenye mkoa wa Morogoro ulioko mashariki mwa Tanzania wakionesha mbinu za kuhesabia namba zilizotengenezwa na mwalimu wao.

Hata hivyo, kuna mifano ya mafanikio

Kwa mujibu wa ripoti kuna sehemu zimepiga hatua na kupata mafanikio kwa mfano:

  • Tanzania imepunguza umaskini kwa watoto, kwa kiwango cha asilimia 46 kati ya mwaka 2000 na 2023 kupitia ruzuku za fedha na programu za kuwawezesha kaya maskini.
  • Bangladesh imepunguza umaskini wa watoto kwa kiwango cha asilimia 32 kupitia uwekezaji katika elimu, makazi bora, umeme, maji na usafi wa mazingira pamoja na kutokomeza kabisa kujisaidia katika maeneo ya wazi kutoka asilimia 17 mwaka 2000 hadi sifuri mwaka 2022.

Umaskini unatishia afya na mustakabali wa watoto

UNICEF imeeleza kuwa umaskini huathiri afya ya mtoto, maendeleo ya kiakili, uwezo wa kujifunza na baadaye hupunguza fursa za ajira. Aidha, watoto wadogo, wenye ulemavu na wanaoishi katika maeneo ya migogoro ndio walio hatarini zaidi.

Ripoti pia imeangazia umaskini wa kipato, ikionesha kuwa:

  • Zaidi ya asilimia 19 ya watoto duniani wanaishi chini ya dola 3 kwa siku.
  • Karibu asilimia 90 yao wako Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kusini mwa Asia.

Katika nchi 37 za kipato cha juu, watoto milioni 50 sawa na asilimia 23 wanaishi katika umaskini wa kiwango sawa na jamii wanamoishi, hali inayozuia ushiriki wao kikamilifu katika maisha ya kila siku.

Ingawa umaskini umepungua wastani wa asilimia 2.5 katika kipindi cha mwaka 2013–2023, nchi kama Ufaransa, Uswisi na Uingereza zimeshuhudia ongezeko la zaidi ya asilimia 20. Slovenia imepunguza umaskini kwa zaidi ya robo kupitia sera imara za mafao ya familia na sheria ya mshahara wa chini.

Wasichana nchini Thailand wanaonesha kuunga mkono maendeleo.

Wasichana nchini Thailand wanaonesha kuunga mkono maendeleo.

UNICEF yatoa wito kwa serikali kuongeza uwekezaji kwa watoto

Ripoti imesisitiza kuwa kumaliza umaskini kwa watoto kunawezekana ikiwa serikali zitachukua hatua madhubuti, ikiwemo:

  • Kufanya kumaliza umaskini wa watoto kama kipaumbele cha kitaifa.
  • Kuingiza mahitaji ya watoto katika sera na mipango ya bajeti.
  • Kupanua huduma za ustawi wa jamii, ikiwemo ruzuku za fedha.
  • Kuimarisha upatikanaji wa elimu, afya, lishe, maji, usafi wa mazingira na makazi.
  • Kukuza ajira zenye staha kwa wazazi na walezi.

Hata hivyo UNICEF imeonya kuwa kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa kunaweza kusababisha vifo vya watoto milioni 4.5 chini ya umri wa miaka 5 kufikia mwaka 2030, na kuacha watoto milioni 6 nje ya shule mwaka ujao, kwa mujibu wa makadirio ya jarida la kitabibu la Uingereza The Lancet.

Huu si wakati wa kupunguza kasi,” amesema Russell. Ni lazima kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuhakikisha watoto wanapata huduma wanazostahili. Uwekezaji kwa watoto ni uwekezaji katika dunia salama na yenye ustawi zaidi kwa kila mtu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *